Diwani aishi sokoni miaka 48

Diwani aishi sokoni miaka 48

Muktasari:

  • Diwani mstaafu wa Kibaya wa CCM wilayami Kiteto mkoani Manyara, Fatuma Msemo amelazimika kuishi katikati ya soko la mji wa Kibaya akisubiri fidia ili ahame kupisha miundombinu hiyo ya huduma ya jamii.

Kiteto. Diwani mstaafu wa Kibaya wa CCM wilayami Kiteto mkoani Manyara, Fatuma Msemo amelazimika kuishi katikati ya soko la mji wa Kibaya akisubiri fidia ili ahame kupisha miundombinu hiyo ya huduma ya jamii.

Akizungumza na Mwananchi katika soko hilo linalotegemewa na wananchi wa Kiteto, diwani huyo aliyestaafu miaka 27 iliyopita amesema amelazimika kuendelea kuishi eneo akisubiri fidia yake.

Fatuma alisema uamuzi huo umetokana na Serikali kumtaka asiendeleze eneo lake bali asubiri fidia lakini kwa miaka 48 sasa hajaipata bado ili ahame eneo hilo.

“Nilikuwa na wazazi wangu miaka ya 1960 iliyopita na baadaye walifariki na kuniacha mimi kwenye nyumba hii na mwaka 1974 wakati Kiteto inazinduliwa viongozi walifanyia sherehe hapa nyumbani na kuweka baadhi ya vitu vyao humu ndani” alisema Fatuma.

Alisema watoto wake 10 aliowazaa wote aliishi nao humo na alipotaka kufanya maendeleo aliambiwa mji unapimwa na eneo lake linaweza kuwa soko na baadaye kuelezwa kuwa yuko eneo la soko akitakiwa kusubiri alipwe fidia lakini mpaka leo hajalipwa bado.

Diwani huyo mstaafu anasema suala hilo linafahamika serikalini kwa muda mrefu lakini hadi sasa hajui hatma yake jambo ambalo limekuwa likimsikitisha.

Nyumba ya familia ya Fatuma Msemo iliyopo katikati ya soko ambapo anaishi na wajukuu na watoto wake. Picha Mohamed Hamad

“Kwa kweli nakufa maskini humu ndani, nyumba siruhusiwi hata kufanya marekebisho yoyote. Nyumba inavuja ila sina pa kwenda, kama ni kufa naona nifie hapa tu kama Serikali itashindwa kunilipa fidia yangu basi,” alisema.

Mtoto wa kwanza wa diwani huyo, Daudi Msemo anasema alilazimika kuacha kazi jijini Dar es Salaam na kuja kuungana na mama yake kudai haki yao bila mafanikio hivyo kumwomba Rais Samia Suluhu Hassan Kuingilia kati ili wapate haki yao.

Anasema hakuna asiyejua kuwa nyumba hiyo ipo kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo kwa makubaliano kuwa wangepeiwa eneo mbadala lakini hadi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa.

Alisema kuna kero ya kuishi katikati ya soko lakini mzazi wake atafanya nini kwani bado anasubiri fidia ili ahame kama zilivyofanya familia nyingine.

“Mama ameanza kuchoka sasa, ameaza kukosa imani na Serikali yake kwani viongozi wengi wamefika na kuelezwa bila mafanikio huku akisema wangekuwa na uwezo angeenda kwa Rais Samia kufikisha kilio chake,” alisema.

Makamu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kiteto, Kassimu Msonde alithibitisha madai hayo na kwamba atalisimamia suala hilo kwenye vikao vya juu vya Halmashauri ya Kiteto.

“Nafahamu huu mgogoro ni wa muda mrefu sana kama ambavyo ulisema na nina uhakika halmashauri yetu tutaufanyia kazi ili haki ipatikane,” alisema.

Baadhi ya wafanyabiashara sokoni hapo waliiomba Serikali kuumaliza mgogoro huo kwani ni hatari kwa usalama wa familia hiyo kutokana na makazi yao kuwa katikati ya soko.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Juliana Peter alisema Serikali iimlipe diwani huyo ili ahame na kwend akuanzish amakazi mapya mahali pengine. “Naamini Serikali na halmashauri wana uwezo wa kumlipa fidia huyu mama ili ahame katikati ya soko kwani ana familia ya watoto na wajukuu ambao wanaishi ndani ya soko jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao,” alisema.

Wilayani Kiteto kumekuwapo migogoro kadhaa ya ardhi kutokana maeneo mengi kutopimwa na kutosimamiwa vyema kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.