Diwani, Meya watofautiana kuliita baraza lililopita kuwa la Chadema

Diwani, Meya watofautiana kuliita baraza lililopita kuwa la Chadema

Muktasari:

  • Diwani wa Kata ya Ngarenaro katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Isaya Doita ametofautiana na Meya wa jiji hilo, Maxmillian Iranqhe kuliita baraza la madiwani lililopita kuwa la Chadema badala ya Baraza la Madiwani wa jiji la Arusha.

Arusha. Diwani wa Kata ya Ngarenaro katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Isaya Doita ametofautiana na Meya wa jiji hilo, Maxmillian Iranqhe kuliita Baraza la Madiwani lililopita la Chadema badala ya baraza la madiwani wa jiji la Arusha.

Doita amesema hayo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo Alhamisi Septemba 9, 2021 kwenye ukumbi wa jiji hilo kuwa sio sawa kusema lilikua baraza la Chadema kwa sababu maamuzi yaliyofanywa yalikua ya baraza zima licha ya Chadema kuliongoza kwa kipindi cha miaka mitano.


Meya huyo alikuwa akitumia neno “Baraza la Chadema” wakati akirejea maamuzi yaliyofanywa wakati huo kuhusiana na mambo mbalimbali yakiwemo utaratibu wa baadhi ya wananchi waliojenga nyumba za biashara eneo la Stendi kubwa na ndogo kuwa na mgogoro wa mara kwa mara kati ya wapangaji na jiji.

Doita ambaye ni miongoni mwa madiwani muda mrefu katika baraza hilo akiwa tayari amelitumikia kwa miaka 10 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kabla ya kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kabla ya uchaguzi Mkuu uliopita akiwa na wenzake kutoka Chadema.


Miongoni mwa madiwani hao ambao walifanikiwa kutetea nafasi zao kupitia CCM ni Diwani wa Kata ya Daraja II, Prosper Msoffe, Diwani wa Kata ya Olasiti, Alex Marti na Diwani wa Viti Maalumu, Veronica Hosea ambaye kwa sasa ni Naibu Meya huku aliyekua Meya, Kalist Lazaro aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga.


“Mstahiki Meya ni vizuri tufahamu kuwa maamuzi yaliyofanywa wakati huo hayakua ya Chadema pekee yao bali yalikuwa ya baraza zima la madiwani wa jiji hili wakati huo nilikua huko lakini nimefahamu ukweli nipo CCM,”amesema Doita.


Diwani wa Kata ya Sinon, Michael Kivuyo amesema ipo haja ya kufanya utafiti wa kina kufahamu mgogoro huo wa muda mrefu unasababishwa na nini ili kuumaliza kwa njia ya amani kwa sababu ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya jiji hilo.


Kwa muda mrefu kumekua na mgogoro kati ya waliojenga, wafanyabiashara ambao ni wapangaji wa maduka hayo na uongozi wa jiji hilo kwa madai kuwa waliojenga wanachukua fedha nyingi kuliko wanawazolipa jiji huku baadhi ya madiwani wakisema muda waliopewa waliojenga kurejesha gharama zao umekwisha.