Dk Bashiru aeleza jinsi CCM inavyotumia dola kubaki madarakani

Muktasari:

  • Dk Bashiru amesema kama chama kilichopo madarakani kitashindwa kutumia dola kubaki madarakani, itakuwa ni uzembe wake.

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema kama chama chochote kinachoongoza serikali kitashindwa kutumia dola kubaki madarakani, itakua ni uzembe wake wenyewe.

Lakini akaonya kuwa kinachotakiwa si kutumia dola kunyanyasa washindani wako.

Dk Bashiru ameeleza hayo katika mahojiano na vyombo vya habari vya kampuni ya IPP, leo Machi 6, 2020 alipotembelea studio za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam.

Dk Bashiru alisema vyama tawala kama Kanu cha Kenya na Unip cha Zambia vilishindwa kutumia nafuu ya madaraka na dola, ndio maana viliondolewa.

“Unashika dola halafu unatumia dola kubaki kwenye dola, halafu akitokea mtu ambaye ana busara zaidi kukwambia usitumie dola kubaki kwenye dola ukamsikiliza, siku ukishatoka hurudi,” alisema Dk Bashiru.

Bashiru alisema hata Chadema, au ACT Wazalendo au CUF wakiingia madarakani watatumia dola vizuri ili wasitoke, na hiyo ndio kazi yake hata yeye kama katibu mkuu wa chama tawala kazi yake ni kuhakikisha wanaitumia dola vizuri kuhakikisha hawatoki madarakani.

“Aliye na dola ananufaika na dola hiyo kubaki madarakani. Huo ni ukweli. Hata Chadema ikiingia kwenye dola kuiondoa kwenye dola itakua ni uzembe wake kwa sababu ana nafuu na faida kuwa na dola,” alisema Dk Bashiru.

“Kinachotakiwa usitumie dola vibaya kunyanyasa washindani wako. Lakini kama unataka kutumia dola kuwavuta watoke waliko waje kwako si ni sawa na kwenye vita; unateka vifaru na bunduki halafu unatumia vifaru hivyo hivyo unakwenda kushambulia. Kwa hiyo wanaosubiri sisi tulegelege katika kutumia dola, watasubiri sana.”

Pamoja na Dk Bashiru kusema haitakiwi kutumia dola kunyanyasa washindani, viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakilalamikia kunyanyaswa, kuzuiwa kufanya shughuli za kisiasa, kukamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka.

Vyama vya upinzani pia vilisusia uchaguzi mdogo katika sehemu kadhaa kutokana na malalamiko dhidi ya watendaji wa Serikali wanaosimamia uchaguzi kutokana na kuwanyima barua mawakala, kutowapa fomu za kugombea, wagombea kukamatwa na malalamiko mengine.

Katika mahojiano hayo, Dk Bashiru alisema kuna nafuu kubwa kwa chama kilichopo madarakani kutumia nguvu za dola kufanya mambo ya kujenga imani kwa wapigakura ili kibaki madarakani, kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa akitumbua watumishi wa umma na kusimamia matumizi ya pesa, kukusanya kodi na kuhakikisha chama chake kinabaki madarakani.