Dk Bashiru asema hatima ya Membe, Kinana na Makamba kujulikana kabla ya Machi 2020

Muktasari:

Hatima ya makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana pamoja na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe itajulikana kabla ya Machi Mosi, 2020.

Dodoma. Hatima ya makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana pamoja na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe itajulikana kabla ya Machi Mosi, 2020.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Februari 24, 2020 na katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally katika mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Watatu hao waliitwa mbele ya kamati ya maadili ya CCM baada ya sauti zao kuenea katika mitandao ya kijamii zikieleza jinsi CCM inavyopoteza mvuto, uendeshaji wa nchi na jinsi chama kilivyoshindwa kuwalinda makatibu huo dhidi ya mtu anayewachafua.

Membe alifika mbele ya kamati hiyo yenye wajumbe wanne mjini Dodoma  baada ya hapo alieleza kufurahishwa na mazungumzo, akisema Mungu alimpa ujasiri wa kuzungumza kile alichotaka kuiambia kamati hiyo na kwamba hakuyumba wala kuyumbishwa katika mahojiano.

Kinana na Makamba walihojiwa na kamati hiyo katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Wengine ambao sauti zao zilisikika katika mkanda huo ni Nape Nnauye, ambaye ni mbunge wa Mtama, William Ngeleja (Sengerema) na January Makamba (Bumbuli) walimuomba radhi Rais John Magufuli.

Katika maelezo yake leo, Dk Bashiru amesema

sababu za kuchelewa kutolewa kwa mapendekezo ya mahojiano na makada hao imetokana na kazi alipewa mwenyekiti wa kamati ndogo ya maadili, Philip Mangula.

“Kamati kuu ilikutana Februari 12, 2020  na kutoa siku saba ambazo zilikwisha Februari 19, 2020  lakini kuna kazi ambayo mzee Mangula alikuwa amepewa.”

“Kazi hiyo ni kwenda kufungua jengo la CCM mkoa wa Geita pamoja na kufanya ziara katika mikoa ya Geita, Shinyanga na Tabora, kwa hiyo asingeweza kukamilisha kwa muda huo,” amesema Dk Bashiru.

Msomi huyo amesema hivi  sasa taarifa imeshakamilisha na kabla ya Machi, 2020 kamati kuu itakutana pamoja na mambo mengine itapokea taarifa ya mapendekezo hayo na wananchi watajulishwa.

Bila ya kutaja adhabu watakayopewa makada hao, Dk Bashiru amesema  kuna makosa mengine yanaweza kutolewa kwa mhusika pekee kwa maana ya onyo, au karipio na adhabu kubwa inaweza kuwa kuvuliwa uanachama au kusimamishwa.