Dk Chaote: Mwili wa Msuya ulikuwa na matundu 26 ya risasi-3

Muktasari:


Agosti 7, 2013 Jiji la Arusha na miji ya Moshi na Mirerani, ilitikiswa na taarifa za kuuawa kwa kupigwa risasi mfanyabiashara maarufu wa madini, Erasto Msuya maarufu kwa jina la Bilionea Msuya, tukio lililotokea wilayani Hai.

Katika mauaji hayo, wauaji wake waliokuwa na pikipiki walitumia mbinu ya kumshawishi kumuuzia madini ya Tanzanite na kumvuta hadi eneo la Orkolili Mijohoroni, ambapo walimminia risasi 22 kwa kutumia bunduki aina ya SMG.

Mwili wake ulikutwa na matundu 26 ya risasi, matundu madogo 13 yakiwa ni sehemu ambayo risasi ziliingia na matundu 13 yalikuwa ya risasi zilipotokea na zilichakaza utumbo mwembamba, kuharibu figo, mishipa ya damu na bandama.

Katika simulizi iliyopita, tulikuletea ushahidi wa mashahidi wawili wa Jamhuri, akiwemo kijana mfugaji wa Kimasai aliyeshuhudia mauaji hayo, Noel Thomas na leo tunakuletea ushahidi wa daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Msuya.
 

Risasi zilivyochana viungo

Shahidi wa upande wa mashitaka, Dk Paul Chaote aliyekuwa Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO), hospitali ya Wilaya ya Hai, alielezea namna alivyoufanyia uchunguzi mwili wa mfanyabiashara huyo na kubaini ulikuwa na matundu 26 ya risasi.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, Dk Chaote alisema Agosti 8, 2013 walipata ombi kutoka polisi la kuufanyia uchunguzi mwili huo ambao uliletwa mochwari Agosti 7, 2013.

“Mwili ulikuwa na migando ya damu katika maeneo mbalimbali ya mwili, ikiwamo mdomoni, masikioni na puani na yalikuwa na majeraha pia. Ulikuwa na jeraha kubwa kichwani na ubongo ulikuwa umetokeza kwa nje,” alieleza Daktari.

Dk alisema kwa kuutazama kwa nje, mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha madogo 13 na majeraha makubwa 13 yaliyosababishwa na risasi.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, uchunguzi huo wa kipatholojia, ulibaini kuwa matundu yale 13 madogo ya risasi ndiko ambako risasi zilizofyatuliwa ziliingilia mwilini wakati matundu makubwa 13 ndiko zilipotokea.

“Majeraha madogo tuliyoyaona katika mwili wa marehemu yaliashiria kuwa risasi zilipigwa kwa umbali mfupi na kule risasi zilipotokea ziliacha uharibifu mkubwa kwa viungo,” alieleza Dk Chaote katika ushahidi ulioibua hisia kwa ndugu.

Shahidi huyo alisema baada ya kuupasua mwili wa marehemu, walikuta utumbo mwembamba umekatika huku risasi hizo zikiharibu figo, mishipa ya damu na bandama lilikuwa limepasuliwa kabisa na mapafu yote mawili yaliharibiwa.

Dk. Chaote alisema mapafu yote mawili yaliharibiwa vibaya kwa risasi, huku mishipa ya damu inayoingia kwenye mapafu, figo na bandama nayo ikiwa imechakazwa vibaya kwa risasi hizo zilizopigwa kwa karibu.

“Kutokana na majeraha hayo, kifo cha marehemu kilitokana na kusimama kwa mfumo wa damu na upumuaji kulikosababishwa na majeraha hayo mabaya ya risasi sehemu mbalimbali za mwili,” alisema Dk Chaote katika ushahidi wake.
 

Mawakili wapinga taarifa ya daktari

Shahidi huyo ambaye baada ya uchunguzi huo aliandaa ripoti, aliomba kutoa ripoti hiyo kama kielelezo cha ushahidi wake na anaweza kuitambua ripoti hiyo kwa kuwa ina mwandiko wake, saini yake na mhuri wa ofisi yake.

Hata hivyo, mawakili Majura Magafu na Emmanue Safari walipinga kupokelewa kwa kielelezo hicho, huku wakili Magafu akisema kisheria, ni lazima ionyeshe jina la aliyeidhinisha kufanyika kwa uchunguzi huo, tarehe na mahali ulipofanyika.

“Kwenye hii ripoti mtu aliyeidhinisha ni OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya) ambalo sio jina na hii inafanya ripoti isiwe kamili hivyo haipokeleki. Kumekuwa na ukiukaji sana siku hizi, hivyo bila jina kuwepo mtu anaweza kuighushi kirahisi,” alisema.

Kwa upande wake, wakili Safari aliunga mkono hoja za kisheria za wakili Magafu kwamba ripoti inayotaka kutolewa kama kielelezo haina jina la mtu aliyeidhinisha kufanyika kwa uchunguzi, lakini pia hakuna fomu namba PF99 iliyoambatanishwa.

Akijibu hoja hizo, wakili wa Serikali mwandamizi, Abdallah Chavulla, alisema pingamizi lililotolewa na mawakili wa utetezi lilikuwa ni dhaifu na halina misingi ya kisheria na sheria imeweka utaratibu wa kupokea taarifa za kitabibu kama hiyo.

Akinukuu kifungu 291(2) cha sheria aliyoinukuu, wakili Chavulla alisema mahakama inaweza kuamua kuwa nyaraka ni halisi (genuine) na kwamba mtu aliyeweka saini ndio anayesimamia hiyo ofisi au ana sifa za kitaalamu.

“Kitu muhimu cha kwanza ni kwamba iwe ni taarifa ya kitabibu, pili taarifa zinazopokelewa zina uhusiano na jambo lililopo mbele yake na taarifa hiyo imesainiwa na mtu kutoka kwenye hiyo ofisi husika,” alisema Chavulla.

“Mheshimiwa Jaji ripoti hii imekidhi matakwa ya kisheria. Lakini hii sheria haijasema kiuhakika hiyo taarifa iandaliweje. Kwa heshima kabisa tunaona mawakili wa upande wa utetezi wanaipotosha mahakama,” alisisitiza.

Akitoa uamuzi mdogo kuhusiana na mabishano hayo, Jaji Salma Maghimbi aliyesikiliza kesi hiyo, alisema baada ya kuzipitia hoja za pande zote mbili haoni mashiko katika hoja za pingamizi hilo, hivyo mahakama inaipokea ripoti hiyo.
 

Mawakili wamweka kiti moto daktari

Baada ya kupokewa kwa kielelezo hicho, mawakili wa utetezi walipata nafasi ya kumuuliza maswali ya dodoso ambapo akijibu maswali ya wakili Ndusyepo, alikiri kuwa yeye sio mtaalamu wa patholojia, ni mbobezi katika kutibu watu.

Akijibu maswali ya wakili Magafu, shahidi huyo alisema yeye sio mtaalamu wa kuchunguza watu waliokufa, na kwamba waliobobea katika suala hilo wanaitwa wataalamu wa Patholojia na kwa Wilaya ya Hai, hakuna mtaalamu huyo.

Dk Chaote akijibu maswali ya wakili Emmanuel Safari, alisema Agosti 7, 2013 alijulishwa na muuguzi aitwaye Agnes Chami juu ya kuletwa kwa mwili wa Bilionea Msuya na kwamba katika chumba cha maiti kulikuwa na watu wengi na tafrani.

Akijibu maswali ya wakili Lundu, Dk Chaote alisema kwa kawaida hufanya uchunguzi wa aina hiyo kwa ombi la polisi na alichojaza baada ya kufanya uchunguzi huo ni kueleza majeraha aliyoyaona katika mwili wa marehemu.

“Nilijulishwa kuwa kulikuwa na maganda ya risasi yanahusishwa na tukio hilo na ndipo mwili ulipopatikana. Hata kama nisingeambiwa kulikuwa na maganda, bado ningetoa maoni haya haya kuwa majeraha yalisababishwa na risasi,” alisema.

Akijibu swali la mzee mshauri wa mahakama aliyetaka kufahamu kama katika uchunguzi wake alikuta mabaki ya risasi kwenye mwili wa marehemu, shahidi huyo alisema hawakukuta na kwa majeraha hayo haiwezekani kuwa alijiua.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kujibu maswali ya mzee mshauri wa mahakama, Jaji aliahirisha kesi hiyo hadi kesho yake ambapo shahidi mwingine alitarajiwa kutoa ushahidi wake.

Kesho tutawaletea ushahidi wa shahidi wa tano wa Jamhuri, Khalid Sankamunge, ambaye ni mganga wa jadi, mkazi wa kijiji cha Limbula, Wilaya ya Kaliua Mkoa wa Tabora, ambaye wauaji wawili walikwenda kwake kupata zindiko wasikamatwe.

Washtakiwa hao wawili walikwenda nyumbani kwake kijiji cha Limbula, Septemba 9,2013 na waliwataja vijana hao wawili kuwa kuwa ni Karim Kihundwa ambaye ni mshtakiwa wa tano na na Sadick Jabir ambaye alikuwa mshtakiwa wa sita.
Usikose kusoma mwendelezo simulizi ya kesi hii kesho