Dk Gwajima, Pembe kushiriki kongamano WD2023 Rwanda

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Doroth Gwajima

Dar es Salaam. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, Riziki Pembe, wanatarajiwa kushiriki kongamano la Deliver 2023 (WD 2023) linalofanyika Julai 17-20, 2023 jijini Kigali, Rwanda.

Kongamano hilo limejikita katika kuangalia usawa wa kijinsia na kuboresha masuala ya afya na ustawi wa wanawake na wasichana.

WD 20233 inatarajiwa kukutanisha takribani washiriki 5000 kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, huku ikiongozwa na kauli mbiu isemayo "Nafasi, mshikamano na suluhisho,” yenye lengo la kuongeza uhamasishaji katika masuala ya usawa wa kijinsia, haki na ustawi wa wanawake na wasichana katika nyanja zote.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Dk Gwajima alisema kongamano hilo linalenga kuunganisha juhudi za wadau mbalimbali ili kujadili na kupata suluhisho la mambo yanayowakabili wanawake na wasichana ili kuimarisha uwajibikaji, ushirikiano na kuleta mabadiliko.

Lengo jingine la DW2023 ni kuhamasisha na kukuza nafasi za raia kushiriki kwenye masuala yanayohusu wasichana па wanawake hususani katika kuongezeana maarifa na kufahamiana kwa ajili ya ushirikiano na kutathmini sera na uwajibikaji kulingana na maazimio yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita.

"Rais Samia ameniamini na kunituma nimwakilishe kwenye mkutano huu ambapo nitaongoza ujumbe wa Tanzania nikiwa na Riziki Juma wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya hapa nchini. Ushiriki wetu utaangazia dhamira ya Tanzania katika kuendeleza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake nchini," alisema.

Alisema katika mkutano huo Tanzania itashiriki katika matukio mbalimbali muhimu ikiwemo ufunguzi na inatarajiwa kutoa salaam sambamba na viongozi wakuu wa nchi nyingine waalikwa.

Pia kutoa mada katika mikutano mahususi na mijadala itakayofanyika Julai 18-20 Mwaka huu ikiwemo mkutano wa pembeni unaoandaliwa na shirika la BRAC kuhusu juhudi za nchi katika kushughulikia changamoto za umaskini kwa wanawake na vijana balehe kukabiliana na umaskini.

Vilevile kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Afrika yanayoratibiwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika, UNECA na Asasi za Kiraia kwa lengo la kujadili changamoto zilizopo barani Afrika ambazo ni kikwazo katika kufikia usawa wa kijinsia.

"Kushiriki katika mkutano wa kizazi chenye usawa (GEF) unaoandaliwa na shirika la UN Women, wenye lengo la kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ahadi za nchi pamoja na majadiliano ya viongozi wa ngazi ya juutakaohusisha mawaziri 50 na mkutano wa wabunge zaidi 100," alisema.

Aliongeza kuwa kupitia mkutano huo Tanzania itapata nafasi ya kutoa taarifa yake ya utekelezaji kuhusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake nchini na kuelezea jitihada zilizofikiwa katika kutekeleza ahadi za nchi kuhusu haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake kwenye jukwaa la kizazi chenye usawa.