Dk Hoseah, tafakari zaidi haya ya Katiba

Muktasari:

  • Mwishoni mwa wiki Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Edward Hoseah alizungumza mambo kadhaa kuhusu suala la mjadala wa Katiba Mpya ambao umeshamiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mwishoni mwa wiki Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Edward Hoseah alizungumza mambo kadhaa kuhusu suala la mjadala wa Katiba Mpya ambao umeshamiri katika maeneo mbalimbali hapa nchini.


Sina budi kuonyesha masikitiko yangu kuhusiana na uchangiaji wake kwenye suala hilo muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu.
Kwa nafasi yake kama kiongozi wa chombo husika, ilibidi aonyeshe njia kama ambavyo uongozi unataka.


Kwanza kabisa kwa akili ya kawaida, ni sawa kweli kuwa na mfumo wa vyama vingi bila kuwa na Katiba inayokidhi matarajio ya mazingira mapya?

Kwa hili hata baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere hakuitendea haki nchi kutokana na yeye kuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia ya vyama vingi, lakini kwenye Katiba hakuona umuhimu wake zaidi ya kubadilisha tu sheria chache.

Dk Hoseah amegusia suala la uelewa wa watu kuhusu Katiba. Hii ni sawa, lakini hapo basi nilitarajia kwanza angezungumzia suala la nchi kujulikana kama ya kijamaa.

Itakidi hiyo kwa mfano inabeba mambo mazito kuhusiana na usimamizi mzima wa mfumo wetu wa kiuchumi kiasi kwamba hadi leo kuna wasiwasi kuhusu imani yetu juu ya soko huria.

Yaani unakuta kila Rais anayeingia madarakani inabidi afanye kazi ya ziada kuwaaminisha watu kuwa Serikali yake inaamini kwa dhati mfumo wa soko huria.
Dk Hoseah katika uchangiaji wake ameendelea kutoa mfano potofu kuhusu nchi jirani ya Kenya na Katiba Mpya wanayotumia.

Eti anadai haijawasaidia sana kutokana na baadhi ya matukio yanayoendelea nchini humo.
Hii kauli si sawa hata kidogo.

Awali kabisa ni vyema kumkumbusha kuhusu mapambano makali ya kudai Katiba mpya Kenya. Katika makundi yaliyofanya kazi kubwa kutoka mwaka 1990 wakati nchi hiyo ni ya chama kimoja ni chama cha wanasheria au LSK.

LSK ilifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mabadiliko na hata ilipotokea kuna mtu ameonewa na kuwekwa mathalani kizuizini, LSK walijitokeza na kumpigania kwa nguvu zote. Waliojipambanua ni kama Paul Muite na Gibson Kamau Kuria.
Hapa kwetu TLS hata kupaza sauti ni mtihani. Kuna mambo mengi sana ya kujifunza kutoka kwa LSK.

Historia ya kudai ukombozi wa pili Kenya haiwezi kutenganishwa na LSK. Zaidi ya hapo, haiwezekani eti Katiba Mpya iliyopatikana Kenya mwaka 2010 ni jambo la kawaida. Hakika bila Katiba Mpya vurugu kila baada ya uchaguzi mkuu ingekuwa habari nyingine.

Hadi wagombea urais wanapeleka madai yao mahakamani na mahakama kweli inatengua ni jambo nadra sana si tu kwa Afrika, bali dunia.
Isitoshe Katiba mpya ya Kenya inatoa nafasi kwa mfumo wa ugatuzi.

Huu mfumo ambao kwa namna nyingine unaweza kuitwa “madaraka mikoani”, umekuwa chachu ya mabadiliko makubwa kwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa nyuma sana kimaendeleo tangu nchi hiyo ipate Uhuru.
Hii ilifaa sana kwa maoni yangu nchini Tanzania.

Nchi hii ni kubwa sana kiasi kwamba kutegemea Serikali kuu isimamie mambo makubwa ni kuitwisha mzigo usiobebeka!
Kwa vyovyote vile nadiriki kusema wananchi wengi wa Kenya pamoja na changamoto mbalimbali, wanachukulia Katiba kama mali yao na si kitu cha watawala tu. Hata Jeshi la Polisi linajua linakabiliwa na mazingira mapya yanayoweza kusababisha kujikuta matatani. Naendelea kusema katika uchangiaji wa Dk Hoseah, nilitegemea kwa mtu kama rais wa taasisi nyeti ya TLS kutokuacha kutoa kilio kuhusu mgombea huru. Hili ni jambo la aibu Tanzania.

Ni haki ya msingi sawia na vyama vingi vya siasa. Hata Mwalimu Nyerere alisema ni muhimu kuruhusu haki hiyo baada ya kurejea kwenye vyama vingi.

Mpaka leo ni marufuku Tanzania pamoja na kesi nyingi za mahakamani. Nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Uganda zimeruhusu.
Pamoja na yote, kwenye Katiba inayopendekezwa jambo hilo lilipitishwa na ilipaswa basi Dk Hoseah hapo kuzungumzia namna ya kusukuma jambo hilo.

Kwake ni kama kitu kisichokuwa na uzito.
Ukitaka kuelewa umuhimu wa suala hilo nchini, chukua tu mfano wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Ushetu utakaofanyika hivi karibuni kufuatia kifo cha aliyekuwa waziri wa ulinzi.
Tumeona CCM wakiendesha kura ya maoni. Kwa upande wa vyama vya upinzani, inaelekea vingi vitasusia.

Dk Hoseah, tafakari zaidi haya ya Katiba

Swali la kujiuliza hapo, vyama vikisusia mpigakura anafanyaje? Anabaki tu na chaguo la CCM? Na haki si ni kwa upande wa kuchagua na kuchaguliwa? Maana yake wananchi wa Ushetu wanakosa haki ya msingi!
Hii inabidi Hoseah alitazame vizuri sana. Matokeo yake ni idadi ya wapiga kura kuzidi kushuka.

Tusisahau pia kuna chaguzi nyingi zinafanyika kwenye ngazi ya udiwani. Kwa mtindo huu hali itakuwa si shwari kabisa.
Kuna maeneo mengi ya kufanyiwa kazi na kama Dk Hoseah anataka akumbukwe, basi namshauri achague eneo maalumu badala ya maneno ya jumla. Kwa mfano, mfumo wetu wa uchaguzi unaitwa kwa Kiingereza ‘winner takes all’. Yaani mshindi wa uchaguzi hata kama ameshinda kwa kura moja tu basi anachukua kila kitu.

Tumeona madhara yake sehemu nyingi hadi watu wanakimbilia mahakamani kila wakati.
Kuna mapendekezo ya muda mrefu na hata tume ya uchaguzi baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 ilishauri ni vyema vyama vya upinzani viunge mkono mfumo wa ‘uwakilishi wa uwiano’ au Proportional Representation.

Huu mfumo unatumika katika baadhi ya nchi, zikiwemo Afrika Kusini na Namibia.
Kwa bahati mbaya vyama vya upinzani ukiondoa UDP havitaki kusikia mabadiliko ya kimfumo wakati ingekuwa na msaada mkubwa kwao.

Ushauri mzuri wa NEC ulipuuzwa.
Rai yangu kwako Dk Hoseah ni kujikita kwenye jambo tofauti kama hilo. Au ubuni basi kitu chako chenye manufaa kwetu!
Andrew Bomani ni Kaimu Katibu Mwenezi wa UDP: [email protected].