Dk Janabi: Watu 132 wawekewa maputo Mloganzila, asilimia 99 ni wanawake

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Yakubi Janabi 

Muktasari:

  • Kwa miezi sita iliyopita, Hospitali ya Mloganzila, imeshatoa huduma ya kuweka puto tumboni kwa watu 132, huku asilimia 99 ikitajwa kuwa ni wanawake, tangu walipoanzisha kutoa huduma hiyo mapema Januari mwaka huu.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi amesema hadi kufikia Juni mwaka huu, Hospitali ya Mloganzila imeshawawekea watu 132 maputo tumboni ili kupunguza uzito, huku asilimia 99, ni wanawake.

“Tunatoa huduma ya kuweka puto tumboni, ili kusaidia kupunguza uzito wa mwili, ambapo huduma hiyo hupatikana kwa watu wenye kilo kuanzia 90 nakuendelea”

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya watu wenye uzito kupita kiasi inaongezeka nchini, huku waathirika wakubwa wakiwa wanawake.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 47 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wana uzito uliopitiliza.

Hata hivyo, tiba hiyo ya kuwekewa puto kwenye tumbo la chakula inaelezwa kuwa bora na yenye matokeo ya haraka zaidi ambapo huduma hizo zilianza kutolewa na Hospitali ya Mloganzila mapema Januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa Dk Janabi huduma hiyo ya kuwekewa puto tumboni, inapatikana kwa Sh5 millioni, na walengwa ni watu wenye uhitaji wa kupunguza uzito uliopitiliza.

Dk Janabi ameyasema hayo leo Juni 10, katika hafla ya kuadhimisha siku ya Uimara wa mwili duniani ‘Global wellness day’ ambayo huadhimishwa kila ifikapo Jumamosi ya pili ya mwezi Juni, huku akisihi watu kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari ili kuimarisha afya zao.

“Sukari kwa sasa imekuwa na waraibu wengi kuliko hata kokeini, heroini; watu siku hizi wanapenda sana kula vyakula vyenye sukari jambo ambalo sio sahihi kwa afya zao,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa kliniki ya moyo ya Doctor's Plaza, Sophia Byanaku; amesema ni muhimu kwa watu kuhakikisha wanajali afya zao, kwa kufanya mazoezi na kuwa na lishe bora.

Aidha baadhi ya madaktari walishauri watu kuwa na tabia ya kupima afya zao mara kwa mara, ili kuhakikisha wanaepukana na magonjwa nyemelezi.

“Watu wawe na tabia ya kupima angalau, hata mara mbili kwa mwezi kwani kwa kufanya hivyo, wanaweza kuepukana na magonjwa ambayo yatawasumbua kwa muda mrefu; magonjwa kama kansa, na mengineyo mengi,” ameeleza Dk Adamu Burawa Kliniki ya Moyo ya Doctor’s Plaza.


Pia ameongeza kwa kueleza, kuwa ni muhimu kwa watu wengi kubadilisha mfumo wao wa maisha kwani takwimu zinaonesha hivi sasa, watoto wengi wamekuwa wakikumbana na matatizo mbalimbali ya kiafya ambayo hutokana na aina ya maisha waliokua nayo.

“Siku hizi watu ni wavivu kufanya mazoezi, hali ambayo inawaathiri mpaka kizazi cha sasa ambapo watoto, ndio maana wengi wanaumwa magonjwa ambayo zamani yalikua yanaonekana ni ya watu wazima,” amesema.

Happiness ambaye ni mmoja kati ya watu waliohudhuria maadhimisho hayo amesema amefarijika kuwa mmoja wa washiriki na ametambua kuwa ni muhimu kwa kila mwanadamu kuhakikisha anapima afya yake angalau hata mara moja au mbili kwa mwezi.