Dk Mpango akerwa ujenzi Hospitali ya Mwanga, atoa maagizo kwa Tamisemi

Muktasari:

 Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ameendelea na ziara Mkoa wa Kilimanjaro

Mwanga. Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango ameeleza kutoridhishwa na ubora wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro na kuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kutuma timu kwa ajili ya kufanya uchunguzi.

Makamu wa Rais amesema hayo, leo Alhamisi Machi 21, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Mwanga, katika stendi ya mabasi wilayani humo, baada ya kutoka kutembelea na kukagua ujenzi wa hospitali hiyo.

Pia, ameonyesha kushangazwa na ujenzi kusimamiwa na mhandisi wa kilimo.

"Nimetoka kuangalia ujenzi wa hospitali, msema kweli mpenzi wa Mungu, sijafurahi kwa sababu tungeweza kufanya zaidi, mkurugenzi urekebishe, kwanza hata hiyo barabara yenyewe ya kwenda hospitali haifanani na barabara ya kwenda hospitali ya wilaya," amesema Dk Mpango

"Tarura (Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini) ipo, Mkuu wa Mkoa waambie Tarura waangalie hicho kipande cha kwenda hapo hospitali, kwa sababu hata ikiisha utapelekaje mgonjwa hospitali kwa namna hiyo," amehoji.

Katika kusisitiza hilo, Dk Mpango amesema,"sijafurahishwa na ubora wa baadhi ya kazi zilizofanyika pale, leo ndiyo nimesikia kwa mara ya kwanza mhandisi Kilimo ndiye anasimamia majengo, hapana.

Mkurugenzi umeshindwa hata kumwambia mkuu wa mkoa au wakurugenzi wenzio ukaazima hata mhandisi wa majengo wakakusaidia wakawa wanakuja kukagua...milango ya hovyo."

Amesema tayari ameagiza Waziri wa Tamisemi kupeleka timu kwa ajili ya uchunguzi na kurekebisha ili hospitali hiyo iweze kukamilika na kuanza kazi, na kwamba kwa watakaobainika kuhusika wachukuliwe hatua. 

"Kwa hiyo nimeagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, ataleta timu hapa, mama Samia anatafuta hizi hela kwa jasho na damu, haiwezekani tumuangushe namna hii, kwa hiyo tutaleta timu hapa na hiyo timu ije mara moja, watafute ubora wa majengo na fedha iliyopotea na wanaohusika wachukuliwe hatua." 

Dk Mpango pia amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu kusimamia ujenzi wa Chuo cha Veta katika Wilaya ya Mwanga ili kuhakikisha kinakamilika na vijana wanaingia kupata mafunzo.

"Nimeambiwa pia Veta ujenzi wake unasuasua, kwa hiyo mkalirekebishe, Mkuu wa Mkoa mkalisimamie hili, yale ambayo yanahitajika Serikali kuu tuleteeni ili vijana hawa wa Mwanga waanze kusoma kwenye veta ya hapa"amesema Dk Mpango.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mwanga, Zahara Msangi tayari Serikali imeshatoa Sh2bilioni kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya na yameshajengwa majengo tisa.

"Serikali imeshatoa Sh2 bilioni na mpaka ikamilike hospitali hii inatarajiwa kutumia Sh7.4 bilioni, majengo tisa yamejengwa likiwamo jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo dawa, jengo la mama na mtoto, wodi ya wagonjwa mchanganyiko, Mochwari (chumba cha kuhifadhia maiti), jengo la kufulia na kuchomea taka," amesema.

Awali, akishiriki kilele cha maadhimisho ya siku ya misitu duniani sambamba na uoteshaji wa miti katika viwanja vya shule ya sekondari Same, Wilaya ya Same, mkoani humo, Dk Mpango ameziagiza taasisi za utafiti wa misitu kote nchini, kuongeza kasi ya kufanya tafiti kwa kutumia teknolojia za kisasa zitakazoweza kutatua changamoto ya uharibifu wa mazingira na rasilimali misitu nchini.

Amesema matumizi ya mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia yanasababisha karibia hekta 469, 420 za misitu kupotea kila mwaka hapa nchini ambapo ni sawa na karibia nusu ya ukubwa wa wilaya hiyo.