Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Mwigulu afichua sababu za kukwama kwa miradi mingine nchini

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba akizungumza muda mfupi baada ya kukamilisha ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa majengo ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) mkoani Mwanza. Picha na Damian Masyenene

Muktasari:

  • Baadhi ya miradi ya maji iliyosimama na kushindwa kutoa huduma Misungwi ni pamoja na Kigongo ulioanza kutekelezwa mwaka 2021 kwa gharama ya Sh6.5 bilioni, Ukiligulu wa Sh32 bilioni utakaonufaisha vijiji 16 na ule wa Ilujamate wenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni yote ikitekelezwa na makandarasi wazawa.

Mwanza. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema vipaumbele vya dharura na madhara ya mvua za El-nino ambazo ziliathiri bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha kuchelewa kwa miradi ya maji inayotekelezwa wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

Mambo hayo siyo tu yameathiri utekelezaji wa miradi ya maji Misungwi, bali athari zake pia zimerudisha nyuma utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati katika maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa miradi ya maji inayotekelezwa wilayani Misungwi ni pamoja na ule wa Kigongo ulioanza kutekelezwa mwaka 2021 kwa gharama ya Sh6.5 bilioni, Ukiligulu wenye thamani ya Sh32 bilioni utakaonufaisha vijiji 16 na ule wa Ilujamate wenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni yote ikitekelezwa na makandarasi wazawa.

Dk Mwigulu ametaja sababu hizo leo Jumapili Septemba 15, 2024, baada ya Mbunge wa Misungwi (CCM), Alexander Mnyeti kuibua hoja ya kutokamilika kwa miradi wilayani humo.

Hoja hiyo imeibuliwa kwenye ziara ya Dk Mwigulu ya kukagua ujenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Mwanza, eneo la Nyang'homango, Usagara wilayani humo.

“Bajeti yetu mwaka wa fedha uliomalizika ni kweli imeathirika kwa sababu ya mvua za El-nino, kuna maeneo hayakuwa na bajeti yake na yameathirika, kwa mfano Hanang, tuliongeza nguvu kwenye mradi wa reli uanze kazi, Bwawa la Mwalimu Nyerere na daraja la Kigongo- Busisi, mradi kama huo ukishafikia hatua hiyo, hautatamani upoe, utatamani umalizike. Utafinya baadhi ya maeneo mengine,” amesema Dk Mwigulu.

Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema miradi ya maji iliyosimama wilayani Misungwi kutokana na mkandarasi kudai fedha, tayari Wizara ya Maji ilishafikisha mahitaji yake ofisi kwake na fedha zimeshaanza kutoka ili kuikamilisha na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

“Kwa hiyo, kuna maeneo tuliyaongezea nguvu haraka zaidi, miradi hii tuliyoona inaweza kuanza kutoa huduma kwa haraka zaidi ilipunguza kasi kwenye maeneo mengine, lakini kwa kuwa hiyo mizigo tumeshaitua, basi tutahakikisha miradi yote inakamilika. Hoja zote tutazibeba kwa uzito unaostahili, waambieni wananchi wenu mama yuko kazini, hakuna kitakachopoa,” amesema.

Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi ameitaja baadhi ya miradi ya maji iliyosuasua na kushindwa kutoa huduma ni pamoja na Kigongo ulioanza mwaka 2021 ukitekelezwa kwa gharama ya Sh6.5 bilioni ulianza tangu 2021 lakini umeshindikana kukamilika.

“Mradi mwingine ni ule wa Ukiligulu wenye thamani ya Sh32 bilioni utakaonufaisha vijiji 16 na ule wa Ilujamate wenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni, yote ikitekelezwa na wakandarasi wazawa,” amesema Samizi.

Mnyeti amesema baadhi ya miradi hiyo imeshindwa kuendelea kutokana na makandarasi kuidai fedha Serikali, huku akimuomba Nchemba alishughulikie ili chuo hicho (TIA) kilichopo kata ya Usagara kipate maji.

“Suala la maji kujaa Usagara yote tutazungumza lakini wananchi wanahitaji maji, mradi uliopo wa Ukiligulu unakwenda polepole kwa sababu mkandarasi anatudai na anayelipa madeni ya Serikali ni wewe (Mwigulu Nchemba), nakuomba ulipe madeni ya mkandarasi ili atuletee maji hapa na chuo hiki kipate maji," amesema Mnyeti.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyang'homango kilichopo chuo cha TIA, Peter Kanyilizu amesema ujenzi wa  chuo katika eneo hilo utasogeza fursa ya kukua kiuchumi kwa wananchi.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo amesema ujenzi wa kampasi hiyo ambayo ni ya nane nchini unagharimu Sh7.8 bilioni.

Utakapokamilika utasaidia TIA kutoka kwenye majengo ya kupanga na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 12,870 mwaka 2016/2017 hadi 28,979 sawa na asilimia 55.6 huku madarasa mapya yakiwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,980 kwa wakati mmoja ukilinganisha na wanafunzi 600 kwenye majengo ya awali.