DK Mwinyi ateua wengine wawili

Muktasari:

Mwinyi amefanya uteuzi huo siku mbili baada ya kuapishwa kuwa mkuu wa visiwa vya Zanzibar baada ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28.

Unguja. Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amemteua Suleiman Ahmed Salum kuwa katibu wake.

Taarifa iliyotolewa leo na katibu wa Baraza la Mapinduzi na katibu mkuu kiongozi, Dk Abdulhamid Yahya Mzee imesema uteuzi huo unaanza kesho, Novemba 5.

Kabla ya uteuzi huo, Suleiman Ahmed Salum alikuwa mkurugenzi msaidizi katika Tume ya Pamoja ya Fedha. Dk Mwinyi amemteua katibu huyo kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Wakati huo huo, Rais Mwinyi amemteua Nahaat Mohammed Mahfoudh kuwa mkurugenzi  mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar.

Kabla ya uteuzi huo, Mahfoudh alikuwa mtumishi wa umma akifanya kazi katika taasisi tofauti za sekta binafsi.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Mwinyi alifanya ziara jana Bandari ya Malindi alikobaini mapungufu kadhaa ya kiutendaji ambayo anataka yafanyiwe kazi haraka.

Wakati wateule hao wakisubiri kuanza kutekeleza majukumu yao, Dk Mwinyi amemwapisha Dk Mwinyi Talib Haji kuwa mwanasheria mkuu wa Zanzibar.

Kabla ya uteuzi huo, Dk Talib aliyeteuliwa jana alikuwa naibu katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.