Dk Mwinyi atoa somo wakaguzi wa ndani

Muktasari:

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi amesema ipo haja  wakaguzi wa ndani kujikita katika vitendo kuliko kufanya ukaguzi vitabu tu.

Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Mwinyi amesema ipo haja  wakaguzi wa ndani kujikita zaidi kwenye utendaji badala ya kuishia kukagua vitabu hatua itakayosaidia kujua matumizi ya fedha za umma yanavyofanyika.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Novemba 29, 2021 Ikulu Zanzibar alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Taasisi ya wakaguzi wa ndani nchini Tanzania.

“Ni vyema kukagua miradi husika badala ya kuishia kwenye vitabu kwani kuna mambo mengi mnaweza msiyabaini lakini mkienda kwenye miradi mtagundua kama kuna ubabaishaji,” alisema

Ameahidi kufanya kazi na taasisi hiyo ili Zanzibar iweze kupiga hatua kwa kiasi kikubwa katika ukaguzi wa ndani.

Amesema licha ya umuhimu wa kuwapo wakaguzi wa ndani katika taasisi za Serikali lakini mara nyingi ripoti za ndani huwa haziridhishi kwasababu ya wakaguzi hao kutokuwa na nguvu.

Ameipongeza taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa makatibu wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hatua ambayo itasaidia kupata uwelewa wa pamoja.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, bila ya kuwapo kwa usimamizi mzuri wa ukaguzi wa ndani, fedha za Uviko-19 na zingine zinazotarajiwa kutolewa zinaweza zikapotea.

Naye Katibu wa Baraza la Mapindzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmed Said alisema kada hiyo inatakiwa kuwa na elimu zaidi na kuendelea kunolewa ili kujifunza mbinu mpya.

Awali Rais na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo,  Zelia Njeza alisema iwapo nchi inataka kuimarisha utawala bora ni vyema suala la ukaguzi wa ndani likapewa kipaumbele.

“Taifa linaweza kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi iwapo ukaguzi wa ndani ukipewa kipaumbele, hata hivyo Tanzania imepiga hatua kwenye suala hilo  katika nchi za Afrika,” alisema