Dk Mwinyi azindua vitambulisho vya wajasiriamali Zanzibar

Dk Mwinyi azindua vitambulisho vya wajasiriamali Zanzibar

Muktasari:

  • Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amezindua vitambulisho vya wajasiriamali ambapo vitawasaidia kurasimisha shughuli zao, kuwatambua kisheria na kukuza mitaji yao.


Unguja. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi amezindua vitambulisho vya wajasiriamali ambapo vitawasaidia kurasimisha shughuli zao, kuwatambua kisheria na kukuza mitaji yao.

Uzinduzi huo umefanyika leo Alhamisi Septemba 23, 2021 katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar amesema vitambulisho hivyo vitawarahisishia kupata huduma mbali mbali ikiwemo mikopo katika taasisi kadhaa za kifedha.

“Kwa hakika leo ni siku ya furaha kubwa kwangu kuona kwamba tumeweza kuitekeleza ahadi tuliyoitoa kwa wananchi na hasa wajasiriamali wadogo hapa Zanzibar ya kuwapatia vitambulisho maalum na vya kisasa,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema mbali na ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni zake, pia ni kuzingatia matakwa ya sheria mbalimbali zinazohusiana na wajasiriamali ikiwemo Sheria namba 7 ya mwaka 2014, ambapo lengo lake ni kuweka mazingira maalum ya kuyasaidia makundi ya wajasiriamali wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Pamoja na hayo, Rais Dk Mwinyi amewahakikishia Wajasiriamali kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuwajengea mazingira bora ya kufanya shughuli zao.

Katika kutekeleza hilo ameanza mazungumzo na wawekezaji  kufanikisha ujenzi wa masoko kwa Wilaya Unguja na Pemba huku akitumia fursa hiyo kuwaeleza kwamba katika kipindi kifupi kijacho Serikali itaanza ujenzi wa masoko katika eneo la Jumbi na Chuini kwa Nyanya.

Naye Waziri wa Ofis ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohamed amesema shughuli ya kuanza kuwasajili wajasiriamali imeanza rasmi tangu Agosti 3, 2021 na wanategemea kusajili wajasiriamali wote waliopo visiwani humo.

Hata hivyo hakutaja idadi yao na wanaotarajiwa kusajiliwa

Kuhusu gharama za kitambulisho hicho, Masoud amesema inategemeana na aina ya mjasiriamali, shughuli anayoifanya na eneo husika.

"Mfano mjasiriamali anayetembeza machungwa atalipia Sh30,000 tu kwa mwaka, lakini yule mwenye kibanda anaweza kulipa Sh50,000 hadi Sh100,000 kulingana na shughuli yake na eneo, kwahiyo wanaangaliwa kabla ya kusajiliwa,” amesema