Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Nchimbi aeleza Tanzania inavyoshughulikia saratani ya ubongo

Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza leo Jumatatu, Julai 13, 2026 alipofungua mkutano wa tisa wa kimataifa wa Jumuiya ya Wataalamu wa Saratani ya Ubongo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SNOSSA) ulioratibiwa na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Muktasari:

  • Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi amesema Tanzania hupokea takribani wagonjwa 45,000 wa saratani kila mwaka, huku watu 29,000 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi ametaja vipaumbele vitano vinavyotekelezwa na vitakavyotekelezwa na Serikali kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza, hususan saratani ya ubongo ikiwemo kuongeza wataalamu bingwa wa magonjwa ya mfumo wa fahamu.

Dk Nchimbi ametaja ajali za barabarani zinazosababisha majeraha ya kichwa, kiharusi na kasoro za mfumo wa fahamu kwa watoto kama tatizo linaloongeza mzigo sekta ya afya.

Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Julai 13, 2026 alipofungua mkutano wa tisa wa kimataifa wa Jumuiya ya Wataalamu wa Saratani ya Ubongo Kusini mwa Jangwa la Sahara (SNOSSA) ulioratibiwa na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.

Mkutano huo umewakutanisha zaidi ya wataalamu, watafiti na wadau wa afya zaidi ha 200 kutoka ndani na nje ya Afrika wakijadili maendeleo ya tiba ya saratani za ubongo na magonjwa ya mfumo wa fahamu.

Dk Nchimbi ametaja vipaumbele hivyo ni kuongeza wataalamu bingwa wa magonjwa ya mfumo wa fahamu, upasuaji wa ubongo, tiba ya mionzi na saratani na kuwekeza zaidi katika teknolojia za kisasa na matumizi ya akili unde (AI) katika huduma za afya.

"Tutaongeza idadi ya wataalamu bingwa wa magonjwa ya mfumo wa fahamu, upasuaji wa ubongo, radiolojia na saratani, kuimarisha hospitali za rufaa kwa vifaa na teknolojia za kisasa,"amesema na kuongeza.

"Pia kubuni mifumo endelevu ya kugharamia huduma za afya; kuimarisha matumizi ya taarifa za kidijitali na akili unde katika tiba na tafiti na kupanua ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi," amesema.

Dk Nchimbi amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuboresha huduma za afya, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto ya ongezeko la magonjwa yanayohusisha mfumo wa fahamu.

Akizungumzia uwekezaji katika sekta ya afya, Dk Nchimbi amesema kwa zaidi ya miaka 30 huduma za tiba ya mionzi zilikuwa zinapatikana katika Taasisi ya Saratani Ocean Road pekee, lakini sasa hospitali tatu za kanda na hospitali binafsi 23 zinatoa huduma hizo, hatua inayorahisisha wananchi kupata matibabu karibu na maeneo wanayoishi.

Aidha, amesema Serikali imeongeza mashine saba mpya za MRI, huku mashine za CT Scan zikifikia zaidi ya 96, zikiwamo zaidi ya 60 zinazomilikiwa na Serikali.

"Tumeendelea kuwekeza kuboresha uwezo wa uchunguzi na matibabu kuanzia ngazi ya huduma za msingi hadi hospitali za rufaa za Taifa. Hata hivyo, changamoto zilizopo zinahitaji ushirikiano wa kikanda na kimataifa," amesema.


Alichokisema Dk Samizi

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi saratani za ubongo na uti wa mgongo ni miongoni mwa magonjwa yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu, teknolojia za kisasa za uchunguzi na matibabu, pamoja na ushirikiano wa wataalamu kutoka fani mbalimbali.

Dk Samizi amesema kwa mujibu wa takwimu za 'Globocan 2022', Tanzania hupokea takribani wagonjwa 45,000 wa saratani kila mwaka, huku watu 29,000 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo ambapo zaidi ya asilimia 70 hugundulika wakiwa hatua za juu, hali inayoongeza ugumu wa matibabu na kupunguza nafasi ya kupona.

"Kwa upande wa saratani ya ubongo na uti wa mgongo bado ni miongoni mwa magonjwa yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu, ingawa ugonjwa huo unawakumba watu wachache ikilinganishwa na aina nyingine za saratani, kwa Tanzania takribani visa vipya 198 na vifo 166 vinavyotokana na saratani hiyo kila mwaka," amesema

Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu ili kukabiliana na upungufu wa wataalamu wa magonjwa ya mfumo wa fahamu na saratani, hivyo Serikali inaendelea kuziba pengo hilo kupitia mpango wa ufadhili wa masomo wa  Samia Suluhu Hassan Scholarship ambao tayari umewanufaisha zaidi ya watumishi wa afya 6,000 katika fani mbalimbali za ubingwa.

Awali Rais wa SNOSSA, Dk Alan Davidson amesema mkutano wa mwaka huu ni mkubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa jumuiya hiyo mwaka 2018.

Amesema tangu kuanzishwa kwake, SNOSSA imejikita kuimarisha huduma za saratani za ubongo na mfumo wa fahamu kupitia mafunzo kwa wataalamu wa afya, tafiti, utetezi na kujenga ushirikiano wa kitaaluma ili kuboresha huduma kwa wagonjwa wa watu wazima na watoto barani Afrika.

"Tangu tulipoanzishwa mwaka 2018, tumejenga mtandao mkubwa wa wataalamu na wadau wa saratani ya ubongo kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali,"amesema na kuongeza

"Tumetoa ufadhili kwa zaidi ya wataalamu 150 kushiriki mikutano na mafunzo, hatua inayochangia kuimarisha huduma za saratani za ubongo na mfumo wa fahamu Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara," amesema Dk Davidson.

Kwa upande wake Mwenyeji wa mkutano huo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa MOI,  Dk Mpoki Ulisubisya amesema saratani ya ubongo inaendelea kuwa miongoni mwa magonjwa yanayotoa changamoto kwa mifumo ya afya Tanzania na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hali hiyo kutokana na wagonjwa wengi kuchelewa kugundulika, uhaba wa huduma za kibingwa na familia kulazimika kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.


Fahamu hii

Saratani ya ubongo ni ukuaji usiokuwa wa kawaida wa chembehai ndani ya ubongo ambao hutengeneza uvimbe.

Uvimbe huu unaweza kuwa wa kawaida (sio saratani) au mbaya (saratani inayoweza kuua.

Wataalamu wa afya wanataja dalili za ugonjwa huo ni maumivu ya kichwa hasa asubuhi au baada ya kulala, na huambatana na kichefuchefu na kutapika

Pia matatizo ya fahamu, kupungua kwa uwezo wa kuona, kusikia, au kuzungumza vizuri na mabadiliko ya tabia mgonjwa akiwa na mhemko wa hisia usio wa kawaida, kuchanganyikiwa, na kupoteza kumbukumbu.

Vilevile udhaifu wa mwili, kupoteza nguvu au kupooza kwa upande mmoja wa mwili (kama mkono au mguu), degedege au mshtuko wa ghafla wa kifafa kwa mtu asiye na historia ya ugonjwa huo.