Dk Salim atunukiwa tuzo ya heshima nchini Cape Verde

Dk Salim Ahmed Salim
Muktasari:
- Rais wa Jamhuri ya Cape Verde, Dk Jose Neves, ametunuku tuzo ya heshima Dk Salim Ahmed Salim, Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), kufuatia mchango wake katika mapambano ya ‘Utu na Uhuru wa Maamuzi’ nchini humo.
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Cape Verde, Dk Jose Neves, ametunuku tuzo ya heshima Dk Salim Ahmed Salim, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na baadaye kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Africa (AU).
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema tuzo hiyo ilipokelewa na Ahmed Salim ambaye ni mtoto wa Dk Salim, katika Sherehe ambayo ilifanyika tarehe 5 Julai 2023, Praia, Cape Verde, mwishoni mwa maadhimisho ya miaka 48 ya uhuru wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tuzo aliyotunukiwa mwanadplomasia hiyo nguli nchini, inalenga kutambua mchango wake wa kujitolea katika kuendeleza mapambano nchini Cape Verde yaliyodai usawa katika kutambua ‘utu na uhuru wa maamuzi.’
"Serikali Tanzania, kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inapenda kutoa pongezi zake za dhati kwa Dk Salim kwa Kutunukiwa tuzo hii adhimu," imesema sehemu ya taarifa hiyo kutoka wizara hiyo yenye kusimamia mahusiano ya kigeni.
Taarifa hiyo imeongeza kwamba wizara inatoa shukurani zake kwa Dk Jose Neves, Rais wa Jamhuri ya Cape Verde, kwa kumuenzi mmoja wa watu wakubwa wa Afrika na Mwanadiplomasia mashuhuri, Dk Salim.