Dk Shein aongoza kumbukumbu kifo cha Karume

Muktasari:

Karume aliuawa Aprili 7, 1972 akiwa katika ofisi za makao makuu ya kilichokuwa Chama cha Afro Shirazi (ASP) Kisiwandui mjini Unguja, ambapo sasa ni ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Zanzibar.

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein jana aliwaongoza wanasiasa, viongozi wa dini pamoja na mamia ya wananchi katika dua maalumu ya kumuombea Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Aman Karume.

Karume aliuawa Aprili 7, 1972 akiwa katika ofisi za makao makuu ya kilichokuwa Chama cha Afro Shirazi (ASP) Kisiwandui mjini Unguja, ambapo sasa ni ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Zanzibar.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria dua hiyo ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd; Waziri Mkuu, Kassim Majawaliwa; Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi; Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Kabla ya viongozi wa dini kusoma dua, ilitanguliwa na kisomo cha hitima kilichoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar, Shekh Saleh Omar Kaab.

Dua na nasaha

Akitoa mawaidha katika hafla hiyo, shekh kutoka ofisi ya Mufti wa Zanzibar, Khamis Gharib aliwasihi waumini kufanya matendo mema wakizingatia kuwa kifo kinaweza kumtokea mtu yeyote na muda wowote.

“Lakini pia siku hii ya leo ni muhimu sana kwetu sisi kumuombea kiongozi wetu ambaye alionekana kupigania haki za wanyonge, hili ni suala muhimu kufanyiwa kwa kiongozi ikiwa na maana tunajali kazi aliyofanya katika kupigania haki,” alisema Sheikh Gharib.

Mufti Mkuu wa Zanzibar, Shekh Kaab alisema suala la kifo linahitaji kila mtu kulitambua na kujua wakati wowote anaweza kuaga dunia, hivyo jamii inapaswa kujiweka tayari kwa kufanya mambo mema.

Alisema ni vyema jamii ikaiga historia nzuri ya Mzee Karume ambaye alipigania haki ya wanyonge huku akisisitiza kuwa suala la dua ni muhimu kufanyiwa kiongozi huyo kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa wananchi katika uhai wake.

Mwakilishi wa Wahindu, Kandia Hadi alisema kwa kuwa Karume alipigania uhuru wa watu wote bila ya kuonyesha ubaguzi, dini yao haina shaka juu ya kumtakia kila la heri huko aliko.

Mama Fatma Karume

Fatma Karume ambaye ni mke wa Karume alisema kuwa pamoja na mumewe kuuawa na wapinga maendeleo, lakini familia yake haitaacha kumkumbuka daima kwa wema aliokuwa akiwaonyesha enzi za uhai wake.

Alisema kuwa pamoja na Mzee Karume kuonekana kuwa Rais, lakini kwa upande wa familia ilikuwa ikipata malezi bora na walikuwa na faraja sana kwa kuwa alikuwa mcheshi kwa kila mtu.

Maua kaburi la Karume

Katika hatua nyingine, viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Zanzibar, Dk Shein; Makamu wa Rais, Samia; Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Idd; mwakilishi wa familia ya Mzee Karume, Balozi Ali Karume na viongozi wa dini na wa vyombo vya ulinzi na usalama walipata nafasi ya kuweka mashada maalumu ya maua juu kaburi ya mwanasiasa huyo.

Maua hayo ambayo zaidi ya kumi yaliweka juu ya kaburi hilo kama ishara ya upendo kwa kiongozi huyo aliyepigania Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 na kuifanya Zanzibar kuwa nchi huru.

Historia fupi ya Mzee Karume

Abeid Amani Karume alizaliwa kitongoji cha Pongwe, Mwera Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Agosti 4, 1905.

Mwanasiasa huyo alikuwa wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto watano ya Amani Karume na Amina binti Kadir (Amina Kadudu). Kati ya ndugu zake hao wanne wa baba mmoja na mama, wanaume walikuwa wawili na wanawake wawili lakini wote walifariki kabla ya mwanasiasa huyo kuuawa mwaka 1972.

Karume katika ndoa

Mara ya kwanza, Karume alifunga ndoa na Pili binti Ahmed Ambari mwanzoni mwa miaka ya 1940 na mkewe wa pili alikuwa Ashura binti Maisara.

Baada ya kutengana na wake hao wawili, Mzee Karume alifunga ndoa na Fatma binti Gulamhussein Ismail (Mama Fatma Karume) mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka 1944.

Ndoa ya wawili hao ilifanyika Bumbwini Misufini na makazi ya Mzee Karume na mkewe huyo yalikuwa mtaa wa Kisimajongoo nyumba namba 18/22 mjini Unguja mkabala na kituo cha polisi hivi sasa.

Mkewe Karume, Fatma alizaliwa Bumbwini mwaka 1929 akiwa ni mtoto wa Gulamhussein Ismail na Mwanasha Mbwana Ramadhani, ambapo wazazi wa Fatma ni wazaliwa wa Bumbwini.

Mama Fatma alijifungua mtoto wa kwanza wa kike aliyeitwa Asha mwaka 1946 lakini alifariki siku ya pili yake ambapo mtoto wa pili waliyezaa na Karume ni Amani Abeid Karume aliyezaliwa Novemba mosi, 1948 huku wa tatu akiwa ni Ali Abeid Karume aliyezaliwa Mei 24, 1950.

Maisha ya kazi

Kabla ya kuwa Rais wa Zanzibar 1964 baada ya kufanyika Mapinduzi yaliyouondoa usultani visiwani hapa, Mzee Karume katika miaka ya 1920 aliwahi kufanya kazi za ubaharia katika meli mbalimbali na kufanikiwa kutembelea nchi nyingi ikiwamo Marekani, Uingereza, Canada, China, Msumbiji, Malawi, Kenya na nyinginezo.

Wazanzibari wanavyomlilia

Mwanasiasa huyo mahiri anakumbukwa na Wazanzibari kutokana na ujasiri wake wa kupigania uhuru wao, maisha bora na demokrasia.

Wanavitaja vitu hivyo vitatu kuwa vilimjengea maadui wengi ambao walipenda kuendelea kuwanyanyasa wananchi, huku wakitaka kuwarejesha walikotoka.

“Inawezekana kabisa kati ya haya mambo matatu mojawapo lilisababisha wabaya wake wamuue mzee huyo, lakini kwa kweli alikuwa mtu mzuri, alisimamia ujenzi wa nyumba bora na pia aliwapenda sana Wazanzibari. Sina hakika kama atajitokeza mwingine wa kufuata nyayo,” anasema Mansour Abdulheri.