Dorothy Semu kukaimu kiti cha Maalim Seif

Dorothy Semu kukaimu kiti cha Maalim Seif

Muktasari:

  • Uongozi wa  ACT-Wazalendo, umesema makamu wa mwenyekiti wa chama hicho, bara Dorothy Semu ana kaimu nafasi ya uenyekiti Maalim Seif  Sharif Hamad  kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Dar es Salaam. Uongozi wa ACT-Wazalendo, umesema makamu wa mwenyekiti wa chama hicho Bara, Dorothy Semu ana kaimu nafasi ya uenyekiti Maalim Seif  Sharif Hamad kwa mujibu wa katiba wa chama hicho.

Semu ana kaimu nafasi hiyo kwa muda miezi 12 baada ya Maalim Seif aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kufariki dunia Februari 17 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa akipatiwa matibabu tangu Februari 9.

Taarifa iliyotolewa  leo Jumatatu, Februari 22, 2021 kwa vyombo vya habari na Katibu wa  Habari, Uenezi, Mahusiano kwa Umma, Salim Bimani anasema  Semu anachukua nafasi hiyo kwa mujibu wa  ibara ya 84(3) na (4) ya katiba ya ACT- Wazalendo ya mwaka 2015 toleo la mwaka 2020.

“84(3): iwapo mwenyekiti wa chama hayupo kwa sababu yoyote ile basi makamu mwenyekiti anayetoka upande mwengine wa muungano tofauti na anaotoka mwenyekiti, na kama makamu mwenyekiti aliyetajwa kwanza naye hayupo, basi makamu mwenyekiti aliyebakia atakaimu nafasi ya uenyekiti.

“Kwa kuzingatia ibara ya 84(4) ya katiba ya ACT- Wazalendo, Semu ataendelea kukaimu nafasi hiyo ndani ya kipindi kisichozidi 12 hadi pale mwenyekiti mpya atakapochaguliwa na mkutano mkuu maalumu wa taifa wa chama hicho,” inaeleza taarifa hiyo.

Kabla ya kushika wadhifa wa umakamu uenyekiti, Semu aliwahi kuwa katibu mkuu wa ACT-Wazalendo nafasi alioiacha mwaka jana katika mkutano mkuu ambapo Ado Shaibu alimrithi.