Doyo atangaza kumrithi Hamad Rashid ADC

Katibu Mkuu wa Chama cha ADC, Doyo Hassan Doyo akitangaza nia ya kugombea nafasi ya uwenyekiti.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Katiba ya ADC kiongozi huongoza kwa vipindi viwili vya miaka mitano baada ya kumaliza hataruhusiwa kugombea.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Doyo Hassan Doyo ametangaza nia ya kugombea nafasi ya uwenyekiti wa chama hicho, kinachoongozwa na Hamad Rashid.

Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho nafasi ya kiongozi ni kuongoza  vipindi viwili vya miaka mitano.

Akizungumza na wanahabari leo Alhamisi Juni 6, 2024, Doyo amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kutokana na uzoefu alioupata kutoka kwa Mwenyekiti wa chama hicho Hamad Rashid Mohamed.

Doyo amesema Mwenyekiti wao ameonyesha ukomavu wa kulinda katiba ya chama, ambayo imeweka utaratibu wa kiongozi kuongoza kwa vipindi viwili.

 “Tunapofuata Katiba za vyama tunaenda kuviimarisha, endapo nitafanikiwa kugombea nafasi hii nitahakikisha naleta mabadiliko makubwa ndani ya chama kuelekea uchaguzi,” amesema.

 “Nimejipanga kuwa mwenyekiti na kurithi mikoba ya Hamad Rashid, nimepata mafunzo kwake ni kiongozi mzoefu na mkongwe, elimu niliyoipata kwake kama nikifanikiwa nina mafunzo na uzoefu mkubwa ikiwemo uvumilivu,”amesema Doyo.

Doyo ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa ADC amesema Juni 11, 2024  atachukua fomu na kuanza kuzunguka kutafuta wadhamini 150, Bara 75 na Zanzibar 75 kabla ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Juni 27 mwaka huu.

Doyo ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho ikiwemo mlezi Kanda ya Kaskazini na Mkurugenzi wa Habari amesema kama wanachama watampitisha ataenda kusimamia ajenda ya watu kupata ajira.

“Nitahakikisha pia chama kinaleta ushindani kwenye chaguzi na kupata viongozi watakaosimamia sheria, upatikanaji wa ajira mabadiliko na kusukuma ajenda nyingine za wananchi,”amesema.

Aliyekuwa mgombea Ubunge Kibaha Mjini katika uchaguzi wa 2020 Scola Kahana ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti akiomba wanachama wa chama hicho kumuunga mkono.

"Chama nakifahamu sana naomba mapokezi yenu na mniunge mkono wanachama na wananchi wote tukashirikiane kuleta mabadiliko," amesema Kahana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa vijana wa ADC,  Ibrahim Pogora amesema  si tamaduni za kawaida mtu anapotangaza nia viongozi wengine kuwepo kwenye tukio hilo, hivyo kama watendaji wana dhamana na Doyo na y kuchukua fomu sio bahati mbaya.

 “Doyo anastahili kuungwa mkono kutokana na historia yake, tunatoa wito kwa wanachama wengine kumuunga mkono kwa kuwa tuna dhamana naye,” amesema Pogora.

Msigwa wengine wakaribishwa

Katika hatua nyingine Doyo amemkaribisha Mchungaji Peter Msigwa na wanachama wengine walioshindwa katika chaguzi za Kanda kujiunga na chama hicho ili kukipa nguvu.

Amesema Msigwa alikuwa ni kiongozi wa Kanda na mbunge kwa miaka 10 ni mtu mwenye uzoefu katika siasa.

 "Tunawakaribisha ndugu zetu waliogongwa kwenye kanda, ndugu yangu Msigwa alikuwa mbunge miaka 10 akija huku atatupa nguvu hata CCM hakuko sawa tunawakaribisha," amesema Doyo.

ADC kinakuwa chama cha pili kumkaribisha Msigwa, kwani Juni 3 mwaka huu, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla CCM naye alimkaribisha Msigwa ndani ya chama hicho, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika soko la Kilombero jijini Arusha.

Mchungaji Msigwa aliyekuwa akitetea nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Nyasa ya Chadema alishindwa na mshindani mwenzake, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu katika uchaguzi uliofanyika Mei 30 mkoani Njombe.