DPP amfutia kesi Lissu na wenzake

DPP amfutia kesi Lissu na wenzake

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeifutia kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleao (Chadema) Tanzania Bara, Tundu Lissu na wenzake watatu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeifutia kesi ya uchochezi iliyokuwa inamkabili Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleao (Chadema) Tanzania Bara, Tundu Lissu na wenzake watatu.


Ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuieleza mahakama hiyo kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.


Lissu na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002, katika kesi ya jinai namba 208/2016.


Mbali na Lissu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliofutiwa mashtaka yao na kuwa huru ni Jabir Idris, Mhariri wa Gazeti la Mawio, Simon Mkina, Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboo.


Washtakiwa hao wamefutiwa mashtaka na yao chini ya kifungu namba 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Sura ya 20, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.


Uamuzi wa kuwafutia kesi hiyo, umetolewa leo, Septemba 22, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Joseph Luambano baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.


Wakili wa Serikali, Ashura Mzava ameieleza  mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi, lakini DPP hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.


Baada ya Mzava kueleza hayo, Hakimu Luambano amesema kupitia kifungu hicho, Mahakama imewafutia mashtaka washtakiwa wanne na kuwaachia huru.


Lissu na wenzake wanakabiliwa na mashitaka matano likiwemo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.


Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja, wanakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.


Miongoni mwa mashtaka hayo ni kwamba, washtakiwa Jabir, Mkina na Lissu,  wanadaiwa kutenda makosa hayo kati  Januari 12 na 14, 2016 jijini Dar es Salaam, ambapo waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar' katika gazeti la Mawio.


Katika shtaka la pili, Jabir, Mkina na Lissu wanadaiwa  Januari 14, 2016 walichapisha  chapisho la uchochezi ili kuleta chuki kwa wananchi.


Shitaka la tatu, linamkabili Mehboob, anadaiwa kupiga chapa gazeti la Mawio na kwamba shtaka hilo ni la kuwachochea wananchi wa Zanzibar kuichukia serikali yao.