DPP atia mguu kwenye sakata la bei ya saruji

Saturday November 21 2020
New Content Item (1)
By Elizabeth Edward

Dar/Dom. Wakati sakata la kupanda kwa bei ya saruji likiendelea kutikisa nchini, Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) Biswalo Mganga ameingilia kati na kutaka uchunguzi wa jinai ufanyike.

Mganga amesema kumekuwa na vitendo vinavyoashiria kuwapo mpango uliosababisha bei ya bidhaa hiyo ipande.

Katika taarifa yake aliyotoa jana, DPP amemwelekeza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa pamoja kuanzisha uchunguzi na kukamilisha kazi hiyo ndani ya siku 30.

Maelekezo hayo ni mwendelezo wa hatua ambazo Serikali imeanza kuchukua kufuatia kupanda kwa bei ya saruji baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuahidi kuanza na hilo muda mfupi baada ya kuapishwa kutumikia nafasi hiyo.

Katika kipindi cha mwezi mmoja bei ya saruji katika mikoa mbalimbali nchini ilipanda ghafla kutoka kati ya Sh13,000 hadi Sh16,000 na kufikia Sh20,000 na zaidi.

Kulingana na taarifa ya DPP bei zimepanda si kwa saruji pekee bali pia vifaa vya ujenzi katika nchini hali inayoashiria utendekaji wa makosa ya jinai katika mnyororo wa uzalishaji, usafirishaji na uuzaji wa bidhaa hizo.

Advertisement

“Hali hii imesababisha bidhaa hizo kuuzwa na kununuliwa kwa bei juu au kutopatikana kabisa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Ikumbukwe kwamba ni kosa la uhujumu uchumi,” alisema DPP.

Alisema kulingana na Sheria ya uhujumu uchumi na uhalifu wa kupangwa sura 200 kifungu cha kwanza mwenye leseni au asiye na leseni ya kufanya biashara ni kosa kukutwa na bidhaa katika mazingira yanayoashiria kuunyima umma fursa ya kuinunua bidhaa husika kwa bei stahiki.

“Pili kuuza bidhaa kwa bei au masharti yaliyo kinyume na sheria na tatu wakati wa kufanya biashara husika kutengeneza kwa makusudi mazingira yanayoweza kusababisha uhaba wa bidhaa katika soko.

“Ongezeko kubwa au kupungua kwa bei kinyume cha sheria na athari katika mgawanyo sawa na usambazaji wa bidhaa katika soko kwa wanunuzi katika eneo husika ni makosa kwa mujibu wa sheria hiyo,” alinukuu vifungu hivyo.

Biswalo alieleza kuwa vitendo vyote hivyo ni kinyume na sheria na endapo wahusia watafikishwa mahakamani na kutiwa hatiani wanaweza kuhukumiwa kifungo cha kati ya miaka 20 hadi 30 gerezani.

Sambamba na hilo mali na bidhaa zitakazohusika katika uhalifu huo huo zinaweza kutaifishwa na mahakama na kuwa mali ya Serikali.

“Kwa mamlaka niliyonayo kwa mujibu wa kifungu cha 9(1) na 17(1) na (2) cha sheria ya Usimamizi wa Mashtaka nimetoa maelekezo haya mahususi kwa DCI na Mkurugenzi wa Takukuru waanzishe uchunguzi wa jinai juu ya tuhuma hizi ndani ya siku 30.

“Baada ya kupokea jalada husika la uchunguzi, nitachukua hatua stahiki za kisheria kwa kuzingatia misingi inayoniongoza kama ilivyoainishwa katika ibara ya 59B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 na sheria nyingine za nchi,” alisema DPP.

Wakati huo huo, mwandishi wetu jijini Dodoma ameripoti ongezeko la bidhaa hiyo licha ya kuwa siku ya mwisho aliyoitoa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa wakuu wote wa mikoa wawe wamejua sababu za saruji kupanda bei.

Akitoa neno la shukrani mara baada ya kuapishwa Novemba 16, 2020 Majaliwa alisema Serikali katika miaka mitano iliyopita imejenga miundombinu, sasa kuna usafiri wa reli kwenda Tanga na Arusha, hivyo haoni sababu ya kupanda bei ya saruji.

“Kwa kuwa Ma-RC (wakuu wa mikoa) wote wapo, nawaagiza hadi tarehe 20, saa nne asubuhi wawe wamekwenda kwenye kila kiwanda cha kuzalisha saruji kwenye maeneo yao na mawakala wa kusambaza saruji kujua sababu za kupanda bei ya saruji.

“Serikali haijaongeza hata kodi, miundombinu ipo, waliotaka gesi tumewapelekea, wanaonunua makaa ya mawe yako. Tunahitaji maelezo ya kwa nini bei ya saruji imepanda na kwa kiasi hicho Muheshimwa Rais naanza na hilo,” alisema Majaliwa.

Kwa mujibu wa wauzaji Saruji ya Twiga inauzwa bei ya jumla Sh19,000 badala ya Sh14,500 kwa mfuko wa kilo 50, wakati Simba na Dangote kwa sasa inauzwa Sh18,000 wakati bei ya zamani ilikuwa Sh14,000 kwa mfuko mmoja.

Katika maduka mengi jijini hapa, saruji iliuzwa kati ya Sh19,000 hadi Sh20,500 kwa mfuko mmoja wenye ujazo wa kilo 50 ambao bei ya kawaida huwa ni Sh15,000 na katika maeneo machache ilikuwa Sh16,000.


Advertisement