EACJ kutoa mwelekeo kesi za kupinga Sheria ya Vyama vya Siasa

Muktasari:

  • Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) itatoa mwelekeo wa kesi mbili zilizofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Tanzania na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo na iliyofunguliwa na vyama vya siasa kuhusu sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019.

Arusha. Majaji watatu wa Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) watatoa uamuzi wa hoja za kubishaniwa katika kesi iliyofunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kupinga Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa wakidai inakiuka mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mbele ya Naibu Jaji Kiongozi, Audace Ngiye, Jaji Charles Nyachae na Jaji Richard Wejuli watasikiliza na kutoa uamuzi wa hoja hizo katika kesi namba 04 ya 2019 ambayo LHRC inapinga sheria hiyo iliyopitishwa Januari 29,2019.

Katika kesi hiyo ambayo itafanyika kwa njia ya mtandao Jumatatu Septemba 13,2021 Kituo cha Sheria kinawakilishwa na Wakili Fulgence Massawe ambaye anadai mkataba ulioanzisha EAC ibara ya 4,6(d),7(2),8(1)(c),27(1),30(1) na 38(2) pamoja na kanuni za mahakama hiyo ibara ya 1(2) na 24 ya mwaka 2013 zimekiukwa.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama hiyo,kesi hiyo ambayo mujibu maombi ni Mwanasheria Mkuu wa serikali, LHRC inadai mabadiliko ya sheria yanazuia demokrasia,utawala bora na haki ya kukusanyika pamoja mambo ambayo ni muhimu kwa nchi wanachama wa EAC.

Hoja za LHRC zinasema kuwa mkataba wa jumuiya hiyo unaweka wazi misingi ya demokrasia,utawala wa sheria,uwajibikaji,uwazi na utawala bora na kwamba Tanzania ilisaini mkataba huo mwaka 2000 ikiahidi kuuheshimu.

Pia Majaji wanne wakiongozwa Jaji Kiongozi wa kitengo cha Awali, Jaji Yohane Masara, Audace Ngiye, Dk Charles Nyawello na Richard Muhumuza watasikiliza kesi namba 3 ya mwaka 2019 lililofunguliwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.

Kesi hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali walalamikaji wanadai mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa inakiuka mkataba wa EAC ibara ya 6(d),7(2),8(1)(c),27(1),30 na kanuni za mahakama ya Afrika Mashariki(EACJ) ibara 1(2) na 24.

Walalamikaji hao wanawakilishwa na mawakili John Mallya na Jebra Kambole wa jijini Dar es Salaam ambao miongoni mwa hoja zinazopingwa ni kuwa sheria hiyo inalenga kuminya uhuru wa shughuli za siasa za vyama vya upinzani na kuminya demokrasia kwa ujumla.


Pia Msajili wa Vyama vya Siasa amepewa nguvu zaidi ya kuingilia utendaji wa shughuli za vyama ikiwemo kupewa kwa maandishi na taasisi ya ndani na nje inayokusudia kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo chama husika.