EDO KUMWEMBE: Matope yanayomsubiri Mnyama pale Zimbabwe kesho

EDO KUMWEMBE: Matope yanayomsubiri Mnyama pale Zimbabwe kesho

Muktasari:

SIKU moja dereva mmoja Mzimbabwe alinichukua hotelini kunipeleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Tukazungumza kuhusu mpira. Alikuwa anaufahamu vyema mpira.

SIKU moja dereva mmoja Mzimbabwe alinichukua hotelini kunipeleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Tukazungumza kuhusu mpira. Alikuwa anaufahamu vyema mpira.

Kitu kimoja alikuwa akiongea kwa maringo zaidi kuhusu taifa lake. Alikuwa anamwaga sifa namna ambavyo Zimbabwe walikuwa na utajiri mkubwa wa wachezaji katika eneo la kiungo. Akanikumbushia pia kuhusu viungo wawili wa Zimbabwe ambao wamewahi kutamba Tanzania. Thaban Kamukoso na Justice Majabvi.

Akaendelea kuongelea kuhusu uwezo wa viungo wao kina Knowledge Musona, Willarde Katsande, Khama Billiat, Marvelous Nakamba anayekipiga Aston Villa na wengineo. Alionekana kujivuna sana alipokuwa akizungumzia eneo hilo huku akidai kwamba katika ukanda huu wa Kusini mwa Afrika hakuna kama wao.

Wakati huu Simba wakisubiri kucheza na Platinum ya Zimbabwe kesho pale Harare Zimbabwe kuna kesi tatu ambazo Simba wana kesi za kujibu kuhusu pambano hili. Suala la kwanza ni uwezo wa soka la Zimbabwe hasa katika eneo hilo ambalo dereva wangu alikuwa anajivunia.

Wazimbabwe wazuri. Ni mafundi wa mpira. Achana na eneo hilo, hakuna mchezaji wa Zimbabwe ambaye amewahi kuja Tanzania halafu akawa galasa. Inaanzia kwa Donald Ngoma, Kamusoko, Bruce Kangwa, Never Tegere na Prince Dube. Hakuna mchezaji ambaye alikuja halafu hakucheza katika kikosi cha kwanza.

Hii ni ishara ya kwanza ya kile kinachowasubiri Simba huko Zimbabwe. Wanakwenda kucheza mechi ya uhakika. Kama walivyocheza dhidi ya Plateau ya Nigeria katika mechi mbili za kwanza, hakika hiki kitakuwa kipimo. Hili halitakuwa pambano dhidi ya timu fulani ya Shelisheli. Hii itakuwa mechi ngumu.

Nigeria na Zimbabwe wametuzidi katika soka. Inawezekana klabu zao zinakosa mipango fulani ya uhakika kama ambavyo sisi tumeamua kuwekeza kwa kuchukua wachezaji wa kigeni lakini ukweli ni kwamba wazawa wao wanatutosha kama ambavyo tuliona pambano la marudiano la Plateau United ingawa walitolewa.

Hapo hapo katika sual la Platinum unajiongeza katika jambo jingine. Wazimbabwe wameitoa Costa do Sol ya Msumbiji. Wameichapa nyumbani na ugenini kwa idadi ya mabao mawili katika kila mechi. Sio jambo dogo. Kumbuka mara ya mwisho Simba walitolewa katika michuano hii na timu ya Msumbiji.

Kama unapuuza ushindi wa Platinum nyumbani na ugenini dhidi ya timu ya Msumbiji jikumbushe kwamba timu ya mwisho kuitoa Simba katika michuano hii ilikuwa inatoka Msumbiji. Soka la Msumbiji lipo juu kuliko letu. Anayeifunga timu ya Msumbiji sio mtu wa kumpuuza.

Kuna jambo jingine ambalo litaikabili Simba katika mechi hii. Wapinzani wao kama wao wenyewe walivyo ni wazi kwamba wamekaribia kiasi kikubwa cha pesa kama watatinga katika hatua ya makundi. Kila timu ambayo inatinga katika hatua ya makundi inachukua Dola 550,000.

Mpira wa Afrika una mambo mengi ndani na nje ya uwanja. Katika mzingira haya unalazimika kufanya mbinu nyingi za ndani na nje ya uwanja kuweza kufikia kitita hiki cha pesa. Platinum wamezikaribia noti hizi kuliko ambavyo Plateau walizikaribia. Tegemea kwamba watazitolea macho kwa kiasi kikubwa hasa unapojikumbusha kuhusu hali mbaya ya uchumi wa Zimbabwe kwa sasa.

Tukiachana na hili Simba pia wanatazamiwa kujiangalia wenyewe kuelekea katika mechi hii. Mechi zao mbili za mwisho za Ligi hazikuwa nzuri sana na zimewaacha mashabiki wakishindwa kujiamini. Ni mechi walizoshinda lakini mashabiki hawakuridhika.

Waliwafunga Mbeya City 1-0 pale Nyanda za Juu Kusini halafu wakaichapa KMC kwa matokeo ya aina hiyo hiyo. Matokeo hayakuwa tatizo, tatizo ilikuwa namna ambavyo walicheza. Hapa kuna mambo mawili ya kisoka.

Mara nyingi wachezaji huwa wanajibu mapigo kutegemeana na aina ya presha ya mechi. Tuombee kwamba wachezaji wa Simba wana tabia hii. kwamba walicheza na Mbeya City na KMC kutokana na aina ya mechi ilivyokuwa. Mechi hii ni nyingine na wanajua jukumu kubwa linalowakabili kuliko mechi za Ligi.

Jambo la pili ambalo hatupaswi kuombea ni kwamba labda Simba wameshuka kiwango kwa sababu tofauti. Mtu mmoja alininong’oneza kwamba pale Msimbazi kuna hisia kuwa wachezaji wa Simba wamechoka kwa sababu wamecheza mechi nyingi mfululizo.

Tatizo hii ni mechi nyingine ndani ya hizi mechi za mfululizo. Labda kwa sababu walipaa mapema kwenda Zimbabwe basi inaweza kuwasaidia. Vinginevyo hawawezi kutolewa katika michuano hii huku wakileta kisingizio cha mechi uchovu. Mashabiki hawatawaelewa.

Faida kubwa ambayo Simba wanayo mpaka sasa licha ya yote niliyoyasema kuhusu kinachowezekana kuwa ‘ubora’ wa Platinum ni ukweli kwamba wao kama ilivyo kwa Plateau hawajacheza ligi kwa muda mrefu.

Ligi yao haijarudi tangu dunia ilipokumbana na janga la Corona. Wanachofanya kwa sasa ni kujaribu kuwa wajanja tu. Mechi dhidi ya Do Sol ilikuwa ni mazoezi mechi. Lakini hapo hapo waliporudi kwao wamecheza mechi mbili za kirafiki kwa ajili ya kujiweka fiti.Simba watumie nafasi hii kuwa bora zaidi kuliko wapinzani wao katika mechi mbili za hatua hii. Dhidi ya Plateau tuliweza kuhisi tu kile ambacho Wanigeria hawa wangekifanya kama wangekuwa fiti kwa asilimia zote. Simba isiwaruhusu Platinum kuwa bora katika mechi zote mbili vinginevyo tutajiuliza maswali zaidi kuhusu ubora wa ligi yetu.

Kila la kheri kwa Mnyama. Wachezaji wa kuamua matokeo wapo. Waliwahi kuamua katika mechi fulani za nyuma ingawa mechi za ugenini kama hizi zilikuwa zinawapa tabu. Hii ni mechi nyingine ngumu ya ugenini katika sahani yao.