EDO yawajengea uwezo ‘wamama wadogo'
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya (mwenye skafu), akishiriki furaha na mabinti waliopata ujauzito wakiwa na umri mdogo, maarufu kama wamama wadogo, kutoka Halmashauri ya Mji wa Ifakara baada ya kufunga mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali yaliyotolewa na Shirika la Enlighten Development Organization (EDO). Picha na Hamida Shariff.
Muktasari:
- Kupitia Shirika lisilokuwaa kiserikali la Enlighten Development Organization (EDO) mabinti hao wamepewa ujuzi na ujasiliamali kwenye ushonaji, utengenezaji wa batiki na sabuni, kilimo cha mboga mboga na matunda, stadi za maisha, afya ya akili na uzazi.
Morogoro. Shirika lisilo la kiserikali la Enlighten Development Organization (EDO) limeendelea kuwajengea uwezo mabinti waliopata ujauzito katika umri mdogo, maarufu kama wamama wadogo, kwa kuwapatia mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali yanayolenga kuwasaidia kujitegemea kiuchumi na kurejesha matumaini ya maisha yao.
Jumla ya wamama wadogo 38 wamehitimu mafunzo yaliyowajengea uwezo katika ushonaji, utengenezaji wa batiki na sabuni, kilimo cha mboga mboga na matunda, stadi za maisha, afya ya akili na uzazi pamoja na ujasiriamali.
Shirika hilo, ambalo lilianza shughuli zake mwaka 2018, limekuwa likitoa mafunzo kwa mabinti waliopata ujauzito katika umri mdogo kwa lengo la kuwapa ujuzi utakaowawezesha kujitegemea badala ya kukata tamaa kutokana na changamoto walizopitia.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa EDO, Benitho Miwando, amesema tangu shirika hilo lianze kutekeleza programu hiyo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara mwaka 2018, zaidi ya wamama wadogo 700 wamenufaika.
Mabinti waliopata ujauzito wakiwa na umri mdogo, maarufu kama wamama wadogo, kutoka Halmashauri ya Mji wa Ifakara, wakionyesha vyeti vyao baada ya kuhitimu mafunzo ya ujuzi na ujasiriamali yaliyotolewa na Shirika la Enlighten Development Organization (EDO), yaliyolenga kuwawezesha kujitegemea kiuchumi. Picha na Hamida Shariff.
Amesema wengi wa mabinti hao walikuwa wamepoteza matumaini ya maisha baada ya kupata ujauzito katika umri mdogo, lakini kupitia mafunzo hayo wamepata ujuzi wa kujiajiri na kuanza upya maisha yao.
“Baada ya kuwapa mafunzo tumekuwa tukiwaunganisha katika vikundi ili waweze kupata fursa mbalimbali, ikiwemo mikopo inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi,” amesema Miwando.
Amesema kwa sasa shughuli za shirika hilo zimejikita zaidi katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, huku mipango ikiwa ni kupanua huduma zake na kuwafikia mabinti wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwenza wa Shirika la AKIFRA la nchini Ujerumani, Josephine Said, amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado kuna changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vitakavyowawezesha wahitimu kutumia ujuzi walioupata mara baada ya kumaliza mafunzo.
Amesema upatikanaji wa vifaa hivyo utasaidia wahitimu kuanzisha shughuli za uzalishaji mali kwa haraka na kuongeza nafasi ya kujitegemea kiuchumi.
Mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Aziza Matola, amelishukuru shirika la EDO kwa kuwapatia elimu na ujuzi ambao amesema umebadili mtazamo wake kuhusu maisha.
Amesema kabla ya kujiunga na mafunzo hayo alikuwa amekata tamaa baada ya kupata ujauzito akiwa na umri mdogo, lakini sasa ana ujuzi wa kushona nguo, kutengeneza sabuni ya maji na batiki, ambao anaamini utamwezesha kujipatia kipato na kuboresha maisha yake.
“Leo nina ujuzi ambao utanisaidia kujitegemea. Ninaamini maarifa haya yatakuwa mwanzo wa maisha mapya na mustakabali wenye mafanikio,” amesema Matola.
Akifunga rasmi mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amewataka wahitimu kutumia ujuzi walioupata kama nyenzo ya kujenga uchumi wao na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
Amesema changamoto walizopitia hazipaswi kuwa sababu ya kukata tamaa, bali ziwe chachu ya kupambana na kujenga maisha bora kupitia fursa walizozipata.
Kyobya pia amewapongeza wahitimu hao kwa uvumilivu na juhudi walizoonyesha katika kipindi chote cha mafunzo, akisema hatua yao ya kuhitimu itatoa hamasa kwa mabinti wengine wanaokabiliwa na changamoto kama hizo kutokata tamaa na kutumia fursa zinazopatikana kubadili maisha yao.
Katika kuunga mkono juhudi za shirika hilo, Kyobya alikabidhi vyerehani viwili kwa viongozi wa EDO ili kuongeza uwezo wa kutoa mafunzo ya ushonaji na kuwafikia wanufaika wengi zaidi kwa ufanisi.