Ekari 2.53 milioni kutoka kwenye hifadhi zatolewa kwa wananchi

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/24 leo. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Serikali imetoa jumla ya ekari 2.53 milioni kwa ajili ya matumizi ya wananchi ambao walionekana kukosa ardhi

Dodoma. Serikali imetoa jumla ya ekari 2.53 milioni kwa ajili ya matumizi ya wananchi ambao walionekana kukosa ardhi.

Mbali na hilo, Serikali imeendelea kulipa fidia kwa wananchi waliotakiwa kuhama kwa ajili ya kupisha hifadhi za ardhi ingawa siyo wote wanasifa za kulipwa kwani wapo waliovamia ambao wanatakiwa kuhama wenyewe.

Akisoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake bungeni leo Mei 25, 2023, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amesema kuwa ardhi hiyo ilimegwa kutoka katika maeneo ya hifadhi.

Kwenye bajeti hiyo Waziri ameomba Sh171.372 bilioni ambalo ni ongezeko la Sh8.2 bilioni kutoka bajeti ya 2022/23 iliyokuwa Sh163.2 bilioni.

“Rais Samia Suluhu Hassan alilidhia kutoa ardhi ekari 2.54 milioni kutoka katika maeneo ya hifadhi ili wapate maeneo ya shughuli za kibinadamu lakini pia kutoa kifuta machozi,” amesema Dk Mabula.

Waziri amewataka wananchi waliovamia maeneo ya hifadhi kuondoka bila kulipwa fidia kwani walifanya hivyo kinyume na sheria.