Elimu magonjwa yasiyoambukiza itolewe nyumba kwa nyumba

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe akizungumza kwenye  mafunzo ya kujikinga na magonjwa ambayo sio ya kuambukiza leo Alhamisi Juni 22, 2023 Jijini Dodoma.

Muktasari:

  • Dk Shekalaghe amewataka watanzania kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi pamoja na kuishi mtindo bora wa maisha ili kujikinga na magonjwa ambayo sio ya kuambukiza.

Dodoma. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk Seif Shekalaghe amewataka watoa huduma za afya nchini kutoa elimu ya magonjwa ambayo sio ya kuambukiza (NCDs) kuanzia ngazi ya chini ili jamii iweze kujitambua na kuchukua tahadhari.

Akizungumza leo Alhamisi Juni 22, 2023 Jijini hapa, katika mafunzo ya huduma za magonjwa ambayo sio ya kuambuliza kwa watoa huduma za afya, Katibu Mkuu huyo amesema suala la magonjwa ambayo sio ya kuambuliza ni tatizo kubwa katika jamii kwa sasa.

Amesema zinahitajika jitihada za pamoja kuhakikisha wanapunguza tatizo hilo kwa kutoa elimu kuanzia ngazi ya chini kwa mabalozi, watendaji na kwenye mikutano ya vijiji ili ujumbe uweze kufika kwa urahisi katika jamii.

“Niwaombe kama kuna sehemu ya  kuwasisitiza ni elimu kwa umma tuwaelimishe wajue magonjwa haya yanasababishwa  na nini ili katika familia kama kuna  mtu mmoja asiongezeke mwingine,” amesema.

Dk Shekalaghe ameongeza kwa kusema: “…usipokazania suala la elimu, mtazidiwa na wagonjwa; hatutaki kufikia huko.”

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amewataka watanzania kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi pamoja na kuishi mtindo bora wa maisha ili kujikinga na magonjwa ambayo sio ya kuambukiza.

“Hatufanyi mazoezi muda wote tupo ofisini, tukitoka hapo tunapanda gari tunaenda nyumbani, ukifika nyumbani unaangalia TV mpaka saa nne na wakati umekaa, chakula unaletewa hapo hapo unaenda kitandani unalala ukiamka asubuhi unapanda gari, unaenda kazini, hakuna mazoezi,” amesema.