Eneo korofi Barabara ya Mafinga – Mtwango latengenezwa

Gari likimwaga kifusi eneo la Mtwango, Kata ya Sawala ambalo hivi karibuni wananchi walirekodi video kuonyesha gari ya wagonjwa lilivyokwama.

Muktasari:

 Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile amesema tayari barabara yalikuwa yanakwamba imetengenezwa

Iringa. Eneo la Barabara ya Mafinga - Mtwango lililokuwa na utelezi hadi kusababisha magari kukwama yakiwamo ya wagonjwa, limengenezwa.

Naibu Waziri wa Uchukuzi  na Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile amewaeleza wakazi wa Mufindi kupitia kundi la WhatsAPP la Mufindi Kwetu, kuwa tayari wamefanyia kazi kero hiyo.

Kihenzile amesema Mafinga - Mtwango ni moja ya barabara muhimu kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi kutokana na kusafirisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara ikiwamo chai na mazao ya misitu.

Awali, baadhi ya wananchi walirekodi video iliyokuwa inaonyesha gari la wagonjwa likivutwa bila mafanikio eneo la Mtwango, Kata ya Sawala, Wilayani Mufindi.

"Limefanyiwa kazi," ameandika Kihenzile huku akituma video inayoonyesha hali ya barabara ilivyo sasa.

Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Yudas Msangi amesema Mafinga - Mtwango ni barabara iliyopo kwenye mpango wa kuwekwa lami mwaka huu.

Amesema kwa siku zaidi ya maroli 30 yamekuwa yakipita barabara hiyo kuelekea Kiwanda cha Mgololo na viwanda vingine.

"Uwezo wa barabara ni kupitisha uzito wa tani kumi lakini malori yanayopita yana uzito wa zaidi ya tani 58," amesema Msangi.