Etihad yataja sababu za kusitisha safari Dar

Muktasari:

Uamuzi huo kwa kiasi kikubwa umechangiwa na hasara ambayo kampuni hiyo imekuwa ikiipata


Dar es Salaam. Shirika la Usafiri wa Anga, l Etihad limesitisha rasmi safari zake kati ya Abu Dhabi na Dar es Salaam.

Sababu ya kusitishwa kwa safari hizo imetajwa na Etihad, kuwa ni hasara iliyopata kwa miaka miwili mfululizo na kulazimika kuanza mkakati mpya wa kiutendaji na uwekezaji.

“Tutasitisha safari zetu za Abu Dhabi – Dar es Salaam kuanzia Oktoba 1 mwaka huu,” Etihad iliijibu Mwananchi kupitia mtandao wa Twitter leo Jumanne Juni 19, 2018.

Baada ya Oktoba 1, abiria waliokuwa wasafiri na Etihad kutoka Tanzania watachukuliwa na ndege za Shirika la Ndege la Kenya (KQ) hadi Nairobi ambapo wataunganishwa na shirika hilo kuelekea Abu Dhabi.

Etihad ilianza safari za kuja Tanzania mwezi Desemba 2015 ikiwa ni kituo cha tatu ndani ya Afrika Mashariki baada ya Nairobi, Kenya na Entebe, Uganda.

Mwaka jana shirika hilo lilisitisha safari za Dallas-Fort Worth, Entebbe, Jaipur, San Francisco, Tehran na Venice kutokana na mkakati mpya.

Pia Etihad ilianzisha safari mpya kwenda Baku nchini Azerbaijan Machi mwaka huu na inatarajia kuanza kwenda Barcelona mwezi Novemba.

Mkakati wa kupitia upya safari za Etihad ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na shirika hilo kuboresha biashara baada ya kupata hasara kwa miaka miwili mfululizo.