Ewura yawataka wamiliki wa vituo vya mafuta kuingia mikataba na waagizaji
Meneja wa Ewura Kanda ya kaskazini, Mhandisi Lorivii Lon’gidu alipokuwa akizungumza na wamiliki wa vituo vya mafuta Kanda ya kaskazini jijini Arusha.
Muktasari:
- Ewura umefikia hatua hiyo baada ya kupokea kilio cha wamiliki wa vituo vya mafuta, kulalamikia kunyimwa nishati hiyo na waagizaji hali inayosababisha uhaba wa bidhaa hiyo katika baadhi ya maeneo.
Arusha. Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), wamewataka wamiliki wa vituo binafsi kuingia mikataba ya kibiashara na waagizaji wa nishati hiyo nchini ili kukabiliana na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu.
Ewura umefikia hatua hiyo baada ya kupokea kilio cha wamiliki wa vituo vya mafuta, kulalamikia kunyimwa nishati hiyo na waagizaji hali inayosababisha uhaba wa bidhaa hiyo katika baadhi ya maeneo.
Hayo yamefikiwa kwenye kikaokazi cha wafanyabiashara binafsi wa mafuta Kanda ya Kaskazini katika kutafuta suluhu ya kudumu la uhaba wa mafuta kwenye vituo.
Wakizungumza kwenye kikao hicho kilichoandaliwa na Ewura, wafanyabiashara hao wamesema kuwa changamoto wanaiona kwenye bei elekezi ya uuzaji wa mafuta kutokana na waagizaji kugomea kuwauzia kwa bei ya jumla wakidai haiwalipi hivyo kuamua kuuza kwa bei ya rejareja.
"Kipindi cha mafuta mengi wanatupigia simu kututaka tukanunue mafuta lakini kipindi hichi cha shida hawataki kutuuzia kwa bei ya jumla wanasema hawana mafuta na badala yake wanauza wao wenyewe kwa bei ya rejareja. Hivyo tunaomba Serikali iwabane hawa waagizaji watuuzie na sisi wafanyabiashara wadogo au iongeze bei maana vituo vyetu vya mafuta vitajiendeshaje," amesema Ardold Msele wa vituo vya Gatan Ltd.
Meneja wa Ewura, Mhandisi Lorivii Lon’gidu amewataka wafanyabiashara hao kuingia mikataba ya kibiashara na waagizaji wa mafuta ili kuuziwa mafuta isiwe hisani bali amri ya kisheria.
"Mikataba ya kibiashara ni muhimu sana katika kazi zenu na itawasaidia ili akikunyima mafuta unaweza kukagua kwenye hifadhi zao na kumlazimisha akuuzie na tena kwa bei elekezi na sisi kama wadhibiti tutapata nguvu ya kuwasaidia," amesema.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka waagiaji wa mafuta kufuata sheria na kanuni na taratibu za leseni ya biashara zao kwa kuhakikisha wanawauzia wamiliki wa vituo bidhaa hiyo bila ubaguzi wala unyanyasaji.
Naye Agnes Mushi wa Kilimanjaro alioomba Serikali kuwakutanisha wadau wote wa mafuta wakiwemo waagizaji na wauzaji kwa ajili ya kujadili kwa pamoja changamoto ya sekta hiyo lakini pia kupata suluhisho la kudumu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaoteseka na mvutano huo.