Fahamu madini 27 ya kimkakati na mahitaji yake soko la dunia

Dar es Salaam. Je unajua hazina ya madini Tanzania na mahitaji yake katika soko la dunia?

Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) umetaja madini saba muhimu na madini 27 ya kimkakati huku matumaini ya awali yakionyesha uwezekano wa kuvuna maeneo mengi nchini.

Kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya 2010, marekebisho ya mwaka 2022 imetoa mamlaka kwa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kuanza kufanya tafiti mbalimbali zinazohusisha taarifa za miamba ya madini ya kimkakati, nishati, viwandani na madini ya vito.

Akizungumza katika ufunguzi wa kongamano hilo jana Oktoba 25, 2023 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kanzidata wa GST, Hafsa Seif amesema kuna viashiria vingi vya kupatikana madini hayo.

“Kuna makundi sita tumeyagawa katika vitalu 322 nchi nzima, ukiangalia vitalu vyote kuna viashiria vya madini hayo mkakati isipokuwa kidogo kundi la nne na tano,”amesema Hafsa.

Kisheria, GST hufanya tafiti kubwa za aina tatu ikiwamo ya jiolojia inayofanyika kuangalia aina ya miamba na madini yaliyopo katika miamba bila kujua kiwango halisi, ambayo imefanyika kwa asilimia 97 ya ardhi yote Tanzania.

Utafiti wa pili ni ule jiokemia unaochambua kwa kina aina ya miamba iliyobainika kupitia tafiti za kijiolojia, ambayo imefanyika kwa asilimia 23 nchi nzima.

Utafiti wa tatu wa Jiofizikia unahusisha makundi mawili wa tafiti picha za anga na utafiti wa ardhini. Utafiti wa ardhini unahusisha njia mbili; ukusanyaji wa data za usumaku na zile za umeme.

Utafiti wa anga unaokusanya data kwa njia ya usafiri wa anga unahusisha picha za ukusanyaji wa taarifa za awali na zile za kina ambazo zimefanyika kwa asilimia 16 tu nchi nzima.

Tafiti hizo zinafanyika katika vitalu 322 vilivyogawanywa katika ardhi ya Tanzania. Kila kitalu kina ukubwa wa kilometa za mraba 2,916.


Mahitaji ya soko


Kwa mujibu wa GST, tafiti za awali zinaonyesha Tanzania ina utajiri wa madini saba ya muhimu ambayo hayaanza kuchimbwa nchini ikiwamo  Phosphate inayozalisha mbolea, Dolomite, Kaolin na Sulfur(madawa ya hospitalini), chuma(nondo), Chokaa(saruji) na Jasi kwa ajili ya ujenzi.

Madini 27 ya kimkakati ni pamoja na Tanzanite, Dhahabu, Silva yanayozalisha vito vya thamani, Tin (mabati), Uranium (umeme, mitambo ya nyuklia), rare earth, Chromium na Quartz (vigae), Platinum (nyembe), makaa(nishati), Almasi (kukatia vioo), Molybdenum (vyuma vizito)na Bauxite (alminiam).

Pia, kuna madini mengine ya manganese kwa mahitaji ya dawa za hospitalini, magnesite (plastiki za simu, labtop, TV, Radio), Lead, Graphite (betri za magari), Lithium (betri za simu, labtop), Helium (gesi ya kuchomea vyuma), Kyanite, Nikeli (bodi za magari), Shaba (nyaya za umeme) na kaboni (hospitalini).


Hali ya uwekezaji

Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, akiba ya mashapo ya Nickeli (mawe ya madini) ni tani milioni 58 katika mradi wa uchimbaji wa Nikeli wa miaka 30 huko Kabanga mkoani Kagera huku utafiti wa miaka mitatu iliyopita wa Kampuni ya Helium One Ltd mkoani Rukwa ukibaini futi za ujazo bilioni 138 za gesi hiyo.

Kampuni ya Faru Graphite Corporation Limited jana ilisema inakusudia kuvuna akiba ya tani milioni 70 zilizopatikana kwa miaka 26 wakati mahitaji ya Dunia yanatarajiwa kufikia milioni sita miaka 12 ijayo kwa ajili ya betri za magari na penseli.

Kwa upande wa Lithium yanayohitajika kwa ajili ya kuzalisha betri za simu, Labtop, mahitaji ya madini hayo kwa mwaka 2030 yatafikia tani milioni 2.4  huku tafiti za Benchmark Mineral Intelligence zikionyesha ifikapo mwaka 2035 nusu ya magari ya abiria yatakuwa yakitumia nishati ya umeme.

Aidha, Tanzania pia ina fursa ya kuvuna madini baharini kupitia uwekezaji wa unaohusisha madini ya Polymetallic manganese Nodules, Polymetallic manganese Sulphides. Cobalt-Rich Ferromanganese crust, yanayohitajika kwenye uzalishaji wa simu, mabetri na mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo.