Faida lukuki ulaji wa tango

Muktasari:

Wagonjwa wa kisukari hupata changamoto ya harufu mbaya mdomo, hivyo wanashauriwa kuweka kipande cha tango mdomoni kwa dakika tano angalau mara tatu kwa siku, ili kuondoa bakteria wanaofanya mdomo kutoa harufu mbaya.


Tango linaweza kutumika kama tunda, mboga na hata dawa kwa kuwa lina faida nyingi mwilini na si kwa wenye kisukari tu bali kwa kila mtu.

Tango limejaa vitamini K, C, B na A, pia zinapatikana nyuzinyuzi na madini ya potasiamu na calcium na manganese, asilimia 95 ya tango ni maji, hivyo huulinda mwili kutokana na ukavu.

Madini hayo huimarisha afya ya mifupa na matatizo ya mifupa yanayohusiana na umri na hupunguza maumivu kwenye viungo na mifupa.

Osteoporosis ni ugonjwa wa mifupa ambao husababisha mifupa kuwa dhaifu na unaweza kusababisha mifupa membamba kuvunjika hata ikiwa umepinda kidogo, hivyo ulaji wa matango husaidia kumaliza au kuzuia tatizo hili.

Pia tango lina polyphenols inyoasaidia kuepusha mtu kupata maradhi sugu, hivyo ni vizuri kutumiwa mara kwa mara kwa kunywa juisi yake, kuchanganya kwenye kachumbari bila kumenya maganda yake, kwani yanabeba virutubisho vizuri. Pia unaweza kuweka kwenye mkate na kuchanganya na maji ya kunywa kuyapa ladha na vitamini.

Wagonjwa wa kisukari hupata changamoto ya harufu mbaya mdomo, hivyo wanashauriwa kuweka kipande cha tango mdomoni kwa dakika tano angalau mara tatu kwa siku, ili kuondoa bakteria wanaofanya mdomo kutoa harufu mbaya.

 Maji yaliyopo kwenye matango huwa kama fagio linalosafisha uchafu mwilini, ulaji wa mara kwa mara huyeyusha mawe kwenye figo, kushusha kiwango cha uric Acid na kufanya figo kuwa na afya.

Pia huzuia saratani, kuimarisha afya ya akili na kupunguza uzito wa mwili kwa kuwa mmeng’enyo huenda vizuri. Kunywa juisi ya tango kila siku husaidia kutibu vidonda vya tumbo.

Pamoja na hayo hulinda seli kutokana na uharibifu unaohusiana na kuzeeka na huzuia baadhi ya saratani kama vile saratani ya tezi dume.

Kula tango moja au zaidi ya moja kwa siku kwa sababu hayana madhara yoyote, zaidi ya kuimarisha na kuboresho kinga ya mwili.

Mwandishi wa makala haya Lucy Johnbosco ni mshauri wa wagonjwa wa kisukari