Familia 20 Dodoma zakosa makazi nyumba zikibomolewa

Muktasari:
- Familia zaidi ya 20 katika Mtaa wa Relini, Kata ya Kizota jijini Dodoma zimekosa makazi baada ya kubomolewa nyumba zao kwa kile kinachodaiwa kujenga kinyume na utaratibu.
Dodoma. Zaidi ya familia 20 katika Mtaa wa Relini, Kata ya Kizota jijini Dodoma zimekosa makazi baada ya kubomolewa nyumba zao kwa kile kinachodaiwa kujenga kinyume na utaratibu.
Tukio hilo limetokea jana Jumanne Julai 19, 2022 ambapo Jeshi la Polisi lilifika kusimamia shughuli hiyo hilo na kulazimika kutumia mabomu ya machozi kufuatia kuzuka kwa taharuki ambapo wananchi walikuwa hawakubaliani na zoezi hilo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Julai 20, 2022, Diwani wa Kizota, Jamali Yaledi amesema jambo hilo linatakiwa liangaliwe upya kwani waathirika zaidi wa jambo hilo ni watu wenye kipato cha chini.
“Maisha ya watu hawa yamezidi magumu kwasababu wengi wamekuja kujenga huku hata chumba kimoja ili kuepuka kulipa kodi lakini leo wanabomolewa nyumba zao tena bila taarifa,” amesema
Naye mkazi wa eneo hilo, Halima Bakari aliyebomolewa nyumba yake amesema alishangaa kuona watu wanabomoa nyumba yake bila taarifa.
“Wanakuja kubomoa bila ya taarifa yoyote, bila kibali chochote tukiulizwa ni kupigwa tu mabomu,” amesema Shukrani Adamu ambaye ni mwathirika wa tukio hilo.
Hata hivyo, wakazi hao wanaendelea kupinga ubomoaji huo wakidai suala la mgogoro huo na Jiji bado liko mahakamani.
Katika bomoabomoa hiyo nyumba 10 zilibomolewa jana huku nyumba 15 zikibomolewa awali na kufanya jumla ya idadi ya nyumba 25 kubomolewa hadi sasa.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Relini, Omary Bangababu amesema hakupata taaarifa zozote za ubomoaji wa nyumba hizo hali iliyosababisha taharuki.
“Kama ni kweli hao wananchi wanazungumzwa ni wavamizi basi watafutiwe maeneo mengine maana wakati sisi tupo kwenye mazungumzo wao wamekuja kubomoa,” amesema