Familia za vigogo 12 kuchunguzwa

Makamu wa Rais, Philip Mpango akiangalia burudan ya ngoma wakati wa kongamano la Wahariri na Wadau wa Uhifadhi Mazingira na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji lililofanyika mkoani Iringa juzi. Picha na OMR

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango ameagiza kushughulikiwa kwa watu zikiwamo familia 12 za viongozi waliovamia na kuchepusha maji Bonde la Ihefu.

Iringa. Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango ameagiza kushughulikiwa kwa watu zikiwamo familia 12 za viongozi waliovamia na kuchepusha maji Bonde la Ihefu.

Amekemea uchepushaji huo kwani umesababisha kutotiririka kwa Mto Ruaha Mkuu kwa zaidi ya siku 130 sasa hivyo kuhatarisha maisha ya viumbe hai na wanyama waliopo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

“Viongozi wa mabonde mpo? Nawaagiza kuchukua hatua leo juu ya waliochepusha maji, narudia tena, wale walioziba Mto Ruaha bila vibali vya matumizi ya maji, bomoeni na mbomoe kwa gharama zao na kwa wale wenye vizuizi nivione vibali, vyao,” aliagiza.

Maagizo hayo yanazigusa familia 12 zilizotajwa kuhusika kuliharibu Bonde la Ihefu zikiwamo viongozi wastaafu na waliopo serikalini. Hoja hiyo iliibuliwa jana kwenye kongamano la wahariri, wadau wa uhifadhi wa mazingira na utunzaji wa vyanzo vya maji lililofanyika Iringa.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alifichua akisema kuna familia 12 zinazojinufaisha kupitia Bonde la Ihefu.

Katika kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Wanahabari Watetezi wa Raslimali na Taarifa (Mecira) kwa kushirikiana na TEF, wadau walitizama videoinayoonyesha kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu na kusababisha wanyama kufa huku ukiathiri uzalishaji wa umeme.

Mwenyekiti wa Mecira, Habibu Mchange alisema unahitajika uamuzi mgumu kuokoa chanzo cha Bonde la Ihefu ambalo lililovamiwa na wawekezaji wanaochepusha maji kwenda kwenye mashamba.

Uchepushaji huo unadaiwa kuwa chanzo cha kukauka kwa Mto Ruaha unaotegemewa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na mabwawa ya umeme likiwamo Mtera, Kidatu na Mwalimu Nyerere (JNHPP) ambalo litaanza kujazwa maji Alhamisi hii likishuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa wenye vibali, nataka kuviona. Ni lazima tujue maji yanayotoka ni kiasi gani na yanarudi kiasi gani,” alisema Dk Mpango na kusisitiza kuwa familia 12 zilizotajwa zitachunguzwa ili hatua za haraka zichukuliwe.

Dk Mpango pia alielezwa kuwa zipo fedha zinazotakiwa kujenga tuta litakalomaliza tatizo hilo lakini kwa zaidi ya miaka sita hazijatumika.

“Wapo viongozi wana maslahi binafsi wanaochangia uharibifu huu wa mazingira. Siamini kama wakulima masikini ndio wenye matrekta yanayoziba mito yetu na kupeleka maji yote kwenye mashamba. Hawa ndio ninao wasema wanywe sumu,” alisistiza.

Hivi karibuni, alisema uharibifu umeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 1980 hadi asilimia 63 mwaka 2018 hivyo kutishia uoto wa asili, ubora wa ardhi na shughuli za kiuchumi zinazoitegemea.

“Tumeshaharibu sana mazingira na sasa yanalipa kisasi, tumeanza kula jeuri yetu,” alisisitiza.


Aviomba vyombo vya habari

Dk Mpango aliziagiza wizara, mikoa, mabonde na taasisi zinazohusika kutekeleza maelekezo ya Serikali kuweka alama za mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kusimamia sheria.

Vilevile, aliwataka wanahabari kuendelea kuelimisha na kuandika habari za uchunguzi zitakazoibua madudu kwenye uhifadhi wa mazingira.

“Waandishi mkiamua kuanzisha kampeni ya kuipeleka jamii sehemu fulani inakuwa hivyo, naomba muendelee kutumia kalamu zenu kuhamasisha utunzaji wa mazingira,” alisema Dk Mpango.

Pia, alizitaka taasisi za Serikali kutoa ushirikiano kwa wanahabari katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Vilevile, alimuagiza Waziri wa Habari, Mawasilianona Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuwaelimisha wanahabari namna watakavyoshiriki mkakati huo wa kulinda mazingira na vyanzo vya maji.

“Ningependa kuona zaidi na zaidi mambo mliyotuonyesha hapa, siku hizi habari za kiuchunguzi zimekuwa nadra. Tunaona tunapopitia vyombo vyenu baadhi ya uchambuzi hauna umakini, na wengine wenu mnapindisha ukweli,” alisema Dk Mpango.

Alisema elimu za mazingira ijikite kutoa taarifa, taratibu, sheria na sera za uhifadhi wa mazingira kwa jamii na akavitaka vyama vya siasa, wazee wa mila na viongozi wa dini kusaidia katika hilo.

“Jamii ione ni wajibu kupanda miti na kutotupa taka kila sehemu,” alisisitiza.

Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni limeonja joto la jiwe kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi baada ya kuwa na mgawo wa maji pamoja na umeme uliosababishwa na ukame uliojitokeza kiasi cha mito kukauka.