Fanya haya ukisherehekea sikukuu ya Idd

Friday May 14 2021
By Bakari Kiango

Dar es Salaam. Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum amewataka waumini wa Kiislamu  kutenda mema ambayo hayatawaingiza kwenye makosa katika sikukuu ya Idd el Fitri.

Pia amewataka kuwapeleka watoto wao kwenye maeneo salama na yanayompendeza Mungu na kutorejea kwenye vitendo vibaya baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani.

Sheikh Alhad ameeleza hayo leo Ijumaa Mei 14,2021 muda mfupi baada ya kumalizika ibada ya swala ya Idd iliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja mkoani Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Ile mipango mibaya iliyopangwa na watoto wa kike na kiume kuchanganyika pamoja  kwenda maeneo mbalimbali ya starehe ikiwemo  katika fukwe  ni jambo la haramu na lisilofaa. Wewe mzazi unayemruhusu binti yako akachanganyika na mtoto wa kiume ni jambo linalomkasirisha Mungu hasa katika siku ya leo.”

“Leo ni siku tukufu mno ya kumtukuza Mungu kuwatembelea yatima, wagonjwa, wasiojiweza ili kuwapa furaha pamoja nasi. Tuungane nao pia ni siku ya kuwatembelea ndugu na jamaa na kusameheana pale mlipokeseana,” amesema Sheikh Alhad.

Naye Majaliwa amesema ,“ mgeni wa rasmi wa sikukuu ya Idd mwaka huu ni Rais Samia Suluhu Hassan atakayekuwa nasi katika baraza kuu la Idd mchana Karimjee. Kwa itifaki za Kiserikali mimi nikiwa msaidizi wake sipaswi kutoa hotuba ya Idd.”

Advertisement

Hata hivyo, Majaliwa amewataka waumini wa dini Kiislamu kuzingatia ujumbe uliyotolewa na Sheikh Alhad akisema umewakumbusha jambo muhimu.


Advertisement