FCC yachunguza mabadiliko Simba

FCC yachunguza mabadiliko Simba

Muktasari:

  • Tume ya Ushindani (FCC) imeanza uchunguzi wa mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu ya Simba ambao inawahusu wadaawa watano.
  • Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na FCC, wadaawa hao ni  Simba Sports Club Holding Company Limited ambaye ni mdaawa wa kwanza, Mo Simba Company Limited (Mdaawa wa pili), Simba Sports Club Company Limited, Simba Sports Club na Mohammed Gulamabbas Hassanali Dewji.

Dar es Salaam. Tume ya Ushindani (FCC) imeanza uchunguzi wa mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu ya Simba ambao inawahusu wadaawa watano.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na FCC, wadaawa hao ni  Simba Sports Club Holding Company Limited ambaye ni mdaawa wa kwanza, Mo Simba Company Limited (Mdaawa wa pili), Simba Sports Club Company Limited, Simba Sports Club na Mohammed Gulamabbas Hassanali Dewji.

Taarifa  ya FCC imesema kuwa mdaawa wa tatu kwa kushirikiana na mdaawa wa kwanza, pili na tano walichukua mali na biashara za mdaawa wanne Tanzania Bara bila kuitaarifa tume hiyo kinyume na sheria ya ushindani  kifungu cha 11 (2), 11 (6) (cha mwaka 2018) na kizingiti cha muunganiko wa makampuni cha mwaka 2017.

"Januari 6 mwaka huu, FCC ilifanya maamuzi kwa kutoa matokeo ya awali kuhusiana na tuhuma zinazowakabili wadaawa wote watano.

"Kitendo cha wadaawa wote watano kushindwa kuitaarifu  FCC juu ya muunganiko huo wa makampuni kilisababisha kuinyima tume hiyo nafasi ya kutekeleza jukumu lake la kisheria la kufanya tathmini  juu ya uhalali  wa muunganiko huo unaotuhumiwa kutotaarifiwa kwake kwa mujibu wa sheria," imesema taarifa hiyo.

Tume hiyo pia imetoa nafasi mtu, kampuni, shirika au taasisi kuwasilisha pingamizi kwa kuwa na sababu za kuaminika  kuwa muunganiko unaotuhumiwa kutekelezwa na wadaawa wote watano bila kutolewa taarifa kwa FCC kumeathiri au unaweza kuathiri maslahi yake.

Kwa upande wake, mwanasheria wa klabu ya Simba, Mhina M. Mhina alikiri kupokea taarifa hiyo kutoka FCC na wanaandaa taarifa rasmi.

“Tunaandaa taarifa kuhusiana na suala hilo, na msemaji wa klabu ataitangaza kwa mujibu wa utaratibu wetu,” alisema Mhina kwa njia ya simu.