Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Filamu ya utalii kutikisa soko la China

Muktasari:

  • Filamu hiyo inayolenga kutangaza utalii katika Mlima Kilimanjaro, imeandaliwa na Mtanzania Ram Ally, mwongozaji wa filamu ambaye alifanikiwa kuuza filamu yake ya Nyara katika mtandao maarufu duniani wa Netflix.

Dar es Salaam. Filamu ya Guardians of The Peak itakayozinduliwa Mei 10, 2025 jijini Dar es Salaam, inatarajiwa kutikisa katika soko la utalii la China huku ikitumika kuunadi uzuri wa Mlima Kilimanjaro katika soko la utalii nchini humo.

Filamu hiyo iliyoandaliwa na Mtanzania, Ram Ally, ambaye ni Mwongozaji wa Filamu, akishirikiana na Mtanzania mwenye asili ya China, Elizabeth Mrembo, itakuwa na maudhui ya Mlima Kilimanjaro yenye lengo la kuhamasisha utalii wa mlima huo duniani hasa mataifa ya Asia.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Aprili 29, 2025, jijini Dar es Salaam, Ram amesema uzinduzi wa filamu hiyo, ni mwendelezo wa alichofanya Rais Samia Suluhu Hassan katika filamu mashuhuri ya "Tanzania: The Royal Tour" iliyotangaza vivutio vya utalii kimataifa.

“Leo tumeanza na soko la China, kesho tutaenda katika mataifa mengine ya kimkakati kunadi vivutio vyetu vya utalii ikiwemo India na Marekani,” amesema Ram, ambaye ni Mtanzania wa kwanza kuuza filamu yake ya "NYARA: The Kidnapping" kwenye mtandao mashuhuri duniani wa Netflix.

Amesema kupitia filamu hiyo, si tu watatangaza utalii lakini pia watavutia jamii na wadau katika kuhamasisha kutunza mazingira ya mlima huo mrefu kuliko yote barani Afrika.

Kwa upande wake, Elizabeth amesema filamu hiyo inatokana na maono ya kutaka kulinda mazingira ya Mlima Kilimanjaro ili uwe alama ya Ulimwengu ya utunzaji wa mazingira.

“Tunataka tulinde mazingira wakati huo huo, tukilinda urafiki wa miaka mingi kati ya Tanzania na China ulioasisiwa na waasisi wa mataifa yetu,” amesema Elizabeth.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka Bodi ya Filamu Tanzania, Joseph Kahama amewapongeza Ram na Elizabeth kwa juhudi walizochukua katika filamu hiyo.

“Tunapozungumzia uhifadhi wa maeneo ya kihistoria kama alivyosema Elizabeth, tunapaswa kuyatunza na kuyalinda maana yanatunufaisha kiuchumi na ni fahari yetu sisi Watanzania,” amesema.

Amewataka watayarishaji wa filamu nchini kutotumia nguvu kubwa katika filamu za mapenzi tu, bali waangalie mambo mengine ya manufaa yatakuyovutia watalii na uchumi.