Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maonyesho ya dhahabu yapaisha idadi ya watalii Kisiwa cha Rubondo

Kaimu Mhifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, Robert Mushi akiwaeleza watalii kutoka Kizimkazi Zanzibar faida za kinyeshi cha Tembo.

Muktasari:

  • Kuongezeka kwa watalii hao kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo matangazo yanayotolewa kwenye matamasha, uwepo wa  maonyesho ya dhahabu na teknolojia ya madini yanayofanyika kila mwaka mkoani Geita.

Geita. Idadi ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo, mkoani Geita, imeongezeka kutoka 1,800 mwaka 2022 hadi kufikia 5,000 mwaka huu, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 177.

Inaelezwa kuwa kuongezeka kwa watalii hao kumetokana na sababu mbalimbali, ikiwemo matangazo yanayotolewa kwenye matamasha, uwepo wa maonyesho ya dhahabu na teknolojia ya madini yanayofanyika kila mwaka mkoani Geita, pamoja na filamu ya "’Royal Tour’ iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza baada ya kupokea timu ya watalii 55 kutoka Suluhu Academy ya Zanzibar, Kaimu Mhifadhi wa Kisiwa cha Rubondo, Robert Mushi amesema ongezeko hilo linaashiria kurudi kwa utalii baada ya athari za janga la Uviko-19. Mushi amesema ongezeko hilo limechangiwa zaidi na watalii wa ndani, ambao kwa sasa mwitikio wao ni mkubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Watalii wanaotembelea kivuko hiki wanapata fursa ya kujionea vivutio vya kipekee, ikiwemo utalii wa kutembea kwa miguu, safari za boti, wa kuvua samaki kwa mkono na kuona sokwe waliozoeshwa,” amesema Mushi.

Hata hivyo, amebainisha changamoto ya ujangili hususan uvuvi haramu ndani ya eneo la Hifadhi katika Ziwa Victoria, unaweza kuathiri mazingira ya kisiwa na kupunguza vivutio vya utalii.

Mmoja wa viongozi kutoka Suluhu Academy, Hassan Hamdu amesema ziara yao Chato imelenga kukuza uhusiano baina ya watu wa Chato na Kizimkazi, pamoja na kuangalia mashindano ya Samia Cup yaliyoanzishwa Chato ili kuona vipaji vilivyopo na kuvichukua kuviingiza kwenye Suluhu Academy.

Mbali na kutembelea Hifadhi ya Rubondo, watalii hao wametembelea Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Chato kuona uwekezaji uliofanywa kwenye sekta ya afya, pamoja na kutembelea kaburi la hayati John Magufuli.

Mkurugenzi wa Salam Camp, Salehe Kassim kutoka Zanzibar, amesema utalii walioufanya kwenye hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo, mbali na kuona vivutio ni fursa ya kukitangaza kwa wageni wanaofika Zanzibar ili waweze kufika na kujionea vivutio vilivyopo, hususan sokwe waliozoeshwa.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), watalii wanaotembelea vivutio vya utalii nchini wameongezeka kutoka 997,873 mwaka 2021/22 hadi kufikia 1,514,726 kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024.