Mfahamu simba ‘Tundu Lissu', historia yake
Muktasari:
- Simba ‘Tundu Lissu’ amepewa jina hilo kwa sababu ya umachachari wake na ukorofi akifananishwa na mwanasiasa Tundu Lissu wa Chadema.
Dar es Salaam. Tumeshazoea wanyama kama mbwa, paka, simba, faru na wengine kupewa majina ya watu maarufu kwenye jamii zetu, lakini mwishoni mwa wiki iliyopita, simba aliyepewa jina la Tundu Lissu ndilo lililotamba kwenye mitandao ya kijamii.
Simba huyo amejizolea umaarufu ndani ya saa kadhaa baada ya kupewa jina hilo na Rais Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi lililofanyika Unguja, visiwani Zanzibar lililobeba kaulimbiu isemayo; ‘Kizimkazi Imeitika.’
Simba ‘Tundu Lissu’ (7) alizaliwa Januari mosi, 2018, Dar es Salaam Zoo, nje kidogo ya jijini la Dar es Salaam, eneo la Mwasonga katika Wilaya ya Kigamboni.
Simba huyu ana asili ya hifadhi mchanganyiko za mapori ya Akiba ya Grumeti na Ikorongo yanayopatikana katika mfumo wa ikolojia ya Serengeti, Kaskazini mwa Tanzania ambako ndiko wazazi wake walitokea kabla hawajahamishiwa Dar es Salaam Zoo. Hivyo simba ‘Tundu Lissu’ unaweza kumwita “born town.”
Mara nyingi hujulikana kwa utulivu wake na anaonekana kufurahia uwepo wa watu wanaomzunguka.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa wanyama wa porini, ‘Tundu Lissu’ ana silika ya kujihami na kwa nadra anaweza kuwa mkali pale anapohisi maisha yake yako hatarini. Tabia hizi zinamfanya kuwa simba wa kuvutia na anayehitaji kuzingatiwa kwa makini katika mazingira yake.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori Tanzania (Tawa), inaonyesha baba yake alizaliwa na kuishi kwenye Pori la Akiba la Grumeti karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku mama yake akiwa na asili ya maeneo ya Ushoroba wa Tarangire-Manyara na alifahamika baadaye kwa kuishi eneo lililohifadhiwa la Makuyuni (Makuyuni Wildlife Park).
Sababu kuitwa Tundu Lissu
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametaja sababu za kumpa simba jina la Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu kuwa ni kutokana na umachachari na ukorofi wa mwanasiasa huyo.
“Nataka niseme jana (Jumamosi) kulikuwa kuna vijiclip vinarushwa kulikuwa kuna simba machachari pale mkorofi kidogo, nikauliza huyu simba mmempa jina? Nikaambiwa bado, nikawaambia muiteni Tundu Lissu kwa sababu alikuwa hatulii kama alivyo mwanangu Tundu Lissu," amesema Rais Samia.
Tundu Lissu mwenyewe afunguka
Wakati Rais Samia akitaja sababu za kutaka simba aitwe jina la Tundu Lissu, mwenyewe amesema kiongozi huyo mkuu wa nchi yupo sahihi kutokana na asili ya ukoo wao.
Lissu alivyotafutwa na Mwananchi kuhusu jina lake kupewa simba, amesema Rais Samia yupo sahihi, kwani yeye amezaliwa kwenye ukoo wa mashujaa wa Kinyaturu, watu waliowahi kuua simba wala ng'ombe na wezi wa ng'ombe wao.
“Kwa Kinyaturu mashujaa hao huitwa 'ahomi' (umoja 'muhomi'). Babu yangu mzaa baba, Mughwai, alikuwa muhomi, aliua simba aliyevamia na kuua ng'ombe wake.
“Baba yangu aliyenizaa, Mzee Lissu naye alikuwa muhomi. Aliua simba mara mbili waliovamia na kuua ng'ombe wake,” amesema Lissu.
Ukiachana na simba huyo, pia wapo wanyama wengine wenye majina ya viongozi akiwemo Faru Magufuli, Faru Majaliwa, Faru Ummy Mwalimu, Faru Janet Magufuli, Faru Balozi Regine Hess na Faru Samia ambaye yupo kwenye mchakato wa mwisho kupewa jina hilo.
Wengine ni Faru Pius Msekwa, Faru Telele, Faru Ndugai, Faru Obama, Faru Sokoine, Faru Lemanya, Faru Hillary Clinton, Faru Semfuko, Faru Mabula na Faru Gloria.
Kwanini majina ya viongozi?
Katika ulimwengu wa sayansi na uhifadhi, ni kawaida baadhi ya wanyamapori hai au waliogunduliwa kupewa majina ya wagunduzi au watu mashuhuri duniani, wakiwemo wanasiasa, wasanii, wanamichezo na wanasayansi kutokana na sababu mbalimbali.
Utaratibu Tanzania wanyama kupewa majina, kwa mujibu wa mamlaka mbalimbali za uhifadhi wamesema kuwa zipo taratibu za mtu jina lake kupewa wanyama au wataalamu kuamua kufanya hivyo kutokana na mchango wa mhusika na sababu nyingine.
Wapo wafalme kama Charles III wa Uingereza, Bill Clinton, John F. Kennedy, Winston Churchil na wengine wengi ambao majina yao yamekuwa yakitumiwa kuita wanyama wa nyumbani na porini.
“Uamuzi wa Rais Samia kumwita simba huyu Tundu Lissu ni jambo la kawaida katika uhifadhi na sasa simba huyo ataendelea kutambulika kwa jina hilo kama ishara kwa Lissu na wadau wengine kuendeleza uhifadhi,” ameeleza mhifadhi mmoja mwandamizi kutoka Tawa ambaye hakutaka jina lake litajwe.