Friends of Lowassa wafunguka mazito

Dar/Mikoani. Kama kuna wakati mgumu ambao Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa amewahi kuupitia, basi ni pale alipoamua kuondoka CCM na kuhamia Chadema, imeelezwa.

Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa Lowassa, Goodluck Ole-Medeye, ugumu huo ulitokana na mapenzi aliyokuwa nayo mwanasiasa huyo kwa CCM.

Lowassa aliihama CCM Julai 28, 2015 baada ya jina lake kukatwa na chama hicho katika kinyang'anyiro cha kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo. Dk John Magufuli ndiye aliyepitishwa kuwa mgombea wa chama hicho.

Lowassa amefariki dunia Februari 10 mwaka huu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu ya shinikizo la damu, matatizo ya mapafu na kujikunja kwa utumbo.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwa Lowassa, Masaki jijini Dar es Salaam leo Jumapili Februari 11, 2023 Ole Medeye aliyekuwa kwenye kundi la marafiki wa Lowassa lililofahamika kama ‘Friends of Lowassa’, amesema Watanzania ndio waliochagiza mwanasiasa huyo afanye maamuzi hayo.

Kundi la Friends of Lowassa lilianzishwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015, likiwa na malengo ya kuongeza ushawishi ndani ya CCM na vikao vyake vya maamuzi kumpitisha Lowassa kuwa mgombea urais.

Ole Medeye aliyehamia Chadema wakati wa wimbo la Lowassa, alisema wakati jina lake linakatwa, Watanzania walionyesha kiu ya kumtaka awe kiongozi wao, ndiyo maana alitafuta jukwaa lingine litakalofanikisha haja ya wananchi.

"Unakumbuka wakati ule alifanyiwa kitendo kibaya na katiba ya chama ilikiukwa na ninaamini hivyo hadi leo, ndiyo maana akaamua kutafuta jukwaa lingine la kuhakikisha anatimiza haja ya kuwatumikia Watanzania kama walivyohitaji," amesema Ole Medeye aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Serikali ya awamu ya nne.

Rafiki yake mwingine wa Lowassa ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi amesema mwaka 2015 ndiyo wakati uliokuwa na hekaheka zaidi katika siasa kwa Lowassa kuliko kipindi kingine chochote.

Hekaheka hizo, amesema zilitokana na uamuzi wa mwanasiasa huyo kuondoka CCM kwenda Chadema.

Karamagi amesema ili usifikie wakati kama huo tena ni muhimu CCM inapofanya uteuzi wa wagombea wake isimuonee mtu.

"Tujaribu kufuata taratibu zetu zote za chama wakati wa uteuzi, tukioneana tutapata upinzani ndani ya chama," amesema Karamagi ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera.

Kwa upande wake, mbunge wa zamani wa Busega, Dk Raphael Chegeni amesema maradhi yaliyosababisha kifo cha Lowassa yamechangiwa na misukosuko ya kisiasa aliyoipitia.

Dk Chegeni pamoja na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Lowassa duniani, amewataka waliomkosea kujitokeza hadharani kumuomba radhi kiongozi huyo.

“Amepitia katika misukosuko ya kila aina, tunamshukuru Mungu hata kwa kufikisha hiyo miaka 70 duniani. Kuna matamko mengine yalikuwa yanasikitisha sana wengine walisema atafia ikulu lakini Mungu humchukua mja wake wakati unapofika, mwanadamu hawezi kumpangia Mungu kwamba nani atangulie,” amesema.

Dk Chegeni amesema, “kuna wengi wameondoka hata kabla yake, baadhi walikuwa wanamsema kwamba yeye (Lowassa) ataondoka kabla, usimtakie mwenzako mabaya na kwenye siasa kuna mapito. Niwaombe wale aliowakosea wamsamehe na kwa wale ambao walikuwa na nia ovu naye wamwombe radhi awasamehe kule aliko.”

Chegeni amesema Lowassa amebeba dhambi ya watu wengine katika mchakato wa kisiasa na alikubali kuwa ngao kutokana na tabia yake ya kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya maisha ya watu wengine, kwa kufanya maamuzi magumu.

“Mwaka 1995 alikuwa na uwezo wa kugombea urais lakini akamwachia rafiki yake Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na akamsapoti na kuwa meneja wake wa kampeni mpaka Kikwete akawa Rais mwaka 2005, hiyo yote ni kwa sababu alikuwa akisema jambo analitekeleza,” amesema.

“Wakati wa mchakato wa mwaka 2015 nilikuwa sehemu ya timu yake ya ndani, tulitembea kote katika nchi hii tukaona jinsi gani Watanzania walionyesha kuwa na kiu kwamba awe Rais ajaye wa awamu ya tano wa nchi hii. Kutokana na utaratibu ndani ya CCM haikuwezekana, pamoja na hayo hakuweza kuipasua CCM,” amesema Dk Chegeni na kuongeza:

“Ninaamini siku tukiwa kwenye NEC ile, kwamba jina lake limekatwa kama angesema mimi (Lowassa) leo naamua kuondoka CCM, yawezekana angekipasua lakini alikiheshimu baada ya kukatwa alibaki akatafakari na kufanya maamuzi kwenda chama kingine bila kuathiri mwenendo wa CCM.”


Alama alizoacha

Dk Chegeni aliyekuwa msaidizi wa kiongozi huyo wakati wa kampeni ya kugombea urais, alisema Lowassa ameacha alama kuu nne ambazo ni kuamini falsafa ya kwamba umasikini si sifa ya uongozi mzuri, elimu ndiyo mkombozi wa mtoto wa masikini, kukubali kubeba lawama na kuipenda CCM.

“Lowassa alipigania ujenzi wa shule za msingi na sekondari kila kata. Pia aliagiza ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma na akaitisha kikao na viongozi wa taasisi za umma akawaambia ambao hawako tayari kutoa fedha waandike barua kujiuzulu, walitoa fedha chuo kikajengwa,” amesema Dk Chegeni.

Alisema Lowassa alikuwa mwalimu wake ambaye amemfundisha kuwa na msimamo, huku akikosoa wanasiasa wa sasa wanakosa msimamo badala yake wamegeuka na kuwa ‘chawa’, jambo ambalo kiongozi huyo hakulipenda.

Si hao tu waliomzungumzia, hata Onesmo Nangole, mbunge wa zamani wa Longido alisema Lowassa ni kama mlima ulioanguka, akieleza kwake alikuwa ni zaidi ya ndugu na kaka yake.

"Nimeumia sana, alikuwa ni mtu wa pekee mwenye kipaji cha pekee, pia mwenye upendo na kila mtu, alipenda nchi yake na alipenda sana maendeleo," amesema.

Alisema Lowassa akiwa mbunge wa Monduli, yeye alikuwa mwenyekiti wa wilaya, hivyo alifanya naye kazi.

"Sifa yake kubwa ni ukarimu, pia mtelekezaji katika majukumu, mkikubaliana ni utekelezaji. Alikuwa mtu wa maneno mafupi vitendo virefu," amesema.

Alisema Lowassa hakupenda kusikia mtu ana shida, alipenda kusaidia na kwenye nafasi mbalimbali za uongozi alizopitia ameacha kumbukumbu nzuri na alama.

"Binafsi niliwahi kuumwa, alinisaidia gharama za matibabu yangu India, aligusa maisha yangu na si kwangu tu, amegusa maisha ya wengi. Kwenye maendeleo, kuwasaidia kinamama kusomesha watoto, kuchangia harambee za makanisa na misikiti,” amesema na kuongeza:

"Alikuwa mtu wa kusaidia tangu akiwa kijana, akaenda serikalini akawa waziri katika wizara tofauti hadi waziri mkuu, alifanya kazi kwa uwajibikaji.

Naye Julius Kalanga alisema Lowassa ni mtu ambaye kila mmoja atamzungumzia kwa namna ya pekee.

"Kwangu mimi ambaye nilipokea nafasi ya ubunge kutoka kwake namkumbuka namna ambavyo hakuwa na chuki,” amesema.

Kalanga alisema, "alikuwa ni mnyenyekevu, muungwana na asiyechukia, amewabeba marafiki na maadui zake kwa wakati mmoja. Tulikuwa tunamshangaa wakati mwingine nyumbani kwake anakaa na watu ambao ni maadui zake kisiasa, lakini yeye hakuwa na chuki, alikuwa mvumilivu, alipenda elimu na kuunganisha watu.”

Alisema anamkumbuka zaidi kwa mambo matatu akiwa diwani mwaka 2010 na 2015.

"Tulipata kiangazi Monduli, wafugaji wengi walipoteza ng'ombe, alichukua hatua akawasiliana na Rais wakati huo ni Jakaya Kikwete, kwa mara ya kwanza wafugaji tulipewa ng'ombe 500.”

"Mwaka 2013 mabwawa mengi Monduli yalipasuka, aliongea na Rais tukapewa Sh3 bilioni za kukarabati na alifanikisha ujenzi wa hospitali bora ya wilaya, aliweza kupambania maisha ya watu," amesema.

Imeandikwa na Juma Issihaka na Imani Makongoro (Dar) na Mgongo Kaitira (Mwanza)