Fursa zaidi kwa wakopaji wa nyumba, TMRC yaongeza mwanahisa


Muktasari:

Absa imejiunga kama mbia wa 19 kwa uwekezaji wa mtaji wa Sh1.62 bilioni

Dar es Salaam. Kujiunga kwa Benki ya Absa Tanzania  kuwa mwanahisa katika taasisi ya utoaji mikopo ya nyumba (TMRC),  kutaongeza kiwango cha benki hiyo kutoa mikopo ya nyumba yenye thamani ya Sh32 bilioni kutoka Sh5 bilioni ya sasa.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Februari 5, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Obedi Laiser katika hafla ya benki hiyo kupokewa rasmi kuwa mwanahisa wa taasisi hiyo.

Laiser amesema kwa wao kujiunga na TMRC kunamaanisha benki hiyo itapata fedha zaidi zitakazoelekezwa kwa wateja kwenye mikopo ya nyumba, hivyo kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba za makazi unaolikabili Taifa.

"Hii itafanya wateja wetu wawe na uwezo wa kupata mikopo ya nyumba mikubwa kwa urahisi na kwa muda mrefu zaidi kutokana na ufadhili wa muda mrefu unaotolewa na TMRC," amesema.

Kuhusu walivyojipanga katika kutoa mikopo hiyo, amesema awali waliweka mikakati ya kutoa mikopo, asilimia 50 waliielekeza kwenye sekta ya nyumba lakini kwa uwezeshaji wa TMRC wanaenda kufikia asilimia zaidi ya 200, huku wakipunguza riba kutegemea na aina ya mkopo atakayoihitaji mteja.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya amesema kujiunga kwa Absa iliyoweka mtaji wa Sh1.6 bilioni kunafanya wanahisa katika taasisi hiyo kufika 19.

"Kutokana na hatua hiyo benki hii sasa itaweza kupata fedha nyingi zaidi kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba kutoka TMRC kama sehemu ya mkakati wake wa kukuza biashara yake kupitia mikopo ya nyumba," amesema.

Mgaya amesema mpaka sasa wanahisa waliopo katika taasisi hiyo wameiwezesha TMRC kuwa na mtaji wa Sh27.5 bilioni.

Hata hivyo, amesema tofauti na benki ambayo si mwanahisa, walio wanahisa wanapata unafuu wa riba kwa hadi asilimia 7.5, huku kima cha chini cha kuwekeza ikiwa ni Sh500 milioni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodi ya TMRC, Theobald Sabi, alizikaribisha benki nyingine kuwa wanahisa ili kuongeza wigo wa ukopeshaji na  kuijengea uwezo zaidi TMRC, hivyo kukuza sekta ya mikopo ya nyumba kwa ujumla.