GBT yaingilia kati kudhibiti uraibu wa kubeti, dalili zikitajwa
Muktasari:
- Kwa sasa, GBT inasimamia kampuni 63 zilizosajiliwa kuendesha michezo mbalimbali ya kubahatisha nchini, huku ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kucheza kwa kiasi na kwa kujali ili kuepusha madhara ya kijamii na kiuchumi yanayoweza kusababishwa na uraibu wa kubeti.
Dar es Salaam. Wakati uraibu wa kubeti ukiendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili vijana wengi nchini, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) imeingilia kati kupambana na tatizo hilo.
Katika mojawapo ya njia za kutafuta suluhisho, imetaja mbinu ya kuwazuia watu kucheza kwa lazima ili kuwasaidia waathirika kuondokana na tatizo hilo na kuwahamasisha kucheza kwa uwajibikaji.
Ofisa Mwandamizi wa Uhamasishaji na Elimu kwa Umma wa GBT, Zena Athmani, akizungumza jana, Julai 12, 2026, katika Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF), maarufu Sabasaba, amesema ili kusaidia jamii, taasisi hiyo imekuwa ikiendesha kampeni mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya kucheza kupita kiasi na kuhamasisha ushiriki wa michezo ya kubahatisha kwa busara.
“Tuna kampeni yetu inayojulikana kama ‘Makinika kijana, kubeti sio ajira’, ambayo inalenga kuwafahamisha vijana kuwa michezo ya kubahatisha ni burudani na si chanzo cha mapato. Burudani yoyote ikizidi huleta madhara,” amesema.
Mbali na kampeni hiyo, GBT pia imeendesha kampeni ya Mlinde Mtoto, inayowahusisha wadau wote wa sekta hiyo kuhakikisha watoto hawashiriki michezo ya kubahatisha.
Kwa mujibu wa Zena, elimu hiyo hutolewa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, tovuti ya GBT pamoja na vipeperushi mbalimbali vinavyolenga kuwaeleza wananchi kuhusu dalili za uraibu na namna ya kujilinda.
Hilo linafanyika wakati GBT ikitumia njia mbili kuu kusaidia watu wenye dalili za uraibu wa kubeti kuacha. Ya kwanza ni pale mtu anayejitambua kuwa ameathirika huandika barua ya kujiondoa kushiriki michezo ya kubahatisha kwa kipindi fulani.
Njia ya pili ni GBT yenyewe, kupitia mfumo wake wa ufuatiliaji, kumzuia kwa lazima mchezaji anayeonekana kucheza kupita kiasi na kumpatia ushauri na elimu kuhusu namna ya kushiriki michezo hiyo kwa kiasi.
“Tunafanya ufuatiliaji wa wachezaji na tunapoona mtu anacheza kupita kiasi, tunaweza kumzuia kushiriki kwa muda na kumpa elimu, kwa sababu chochote kikizidi kina madhara,” amesema.
Hizi hapa dalili
Akizungumza na Mwananchi katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Zena amesema ili mtu ajijue kuwa ana uraibu, anapaswa kujiuliza maswali kadhaa.
Miongoni mwa dalili hizo ni mtu kuwa msiri kuhusu kucheza kwa marafiki na ndugu, kujisikia mwenye hatia baada ya kucheza, kukopa fedha ili kubeti, kushindwa kulipa bili na majukumu mengine kwa sababu ya kucheza au kucheza kwa lengo la kurejesha fedha zilizopotea.
Dalili nyingine ni kucheza mpaka fedha zote ziishe, kushindwa kuacha au kupunguza kucheza licha ya jitihada za kufanya hivyo, kushindwa kuhudumia familia kutokana na matumizi makubwa kwenye kubeti na kuathirika kwa utendaji wa kazi.
Pia, mtu anaweza kuwa na uraibu iwapo anagombana na watu wake wa karibu kuhusu kiasi cha fedha anachotumia kucheza, anacheza kwa muda mrefu kuliko alivyopanga au anatumia fedha nyingi kuliko uwezo wake wa kifedha.
“Mtu akiwa anatawaliwa na mawazo ya kucheza kila siku, kutaka kurejea kucheza baada ya kushinda au kupoteza fedha na kutumia michezo ya kubahatisha kama njia ya kupata fedha za kulipia gharama za maisha ni baadhi ya viashiria vya tatizo hilo,” amesema Zena na kuongeza:
“Kama jibu ni ndiyo katika mojawapo ya maswali hayo, basi mtu huyo ana tatizo la kutocheza kwa busara na anapaswa kutafuta msaada,” amesema.
Namna GBT inavyodhibiti ‘madubwi’
Mbali na mchezaji mmoja mmoja, GBT pia imezungumzia mashine za michezo ya kubahatisha maarufu kama madubwi, ikisema kisheria mashine hizo zinapaswa kusajiliwa na kuwekwa katika maeneo maalumu yanayotambuliwa na sheria, ikiwemo kwenye slot shops na baadhi ya maeneo ya biashara yaliyoruhusiwa.
Amesema mashine zinazowekwa kwenye saluni, nyumba za watu au maeneo yasiyoruhusiwa ni haramu.
Kutokana na GBT kutokuwa na uwezo wa kufika katika kila kijiji na mtaa nchini, amesema wameingia makubaliano na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili kusaidiana katika usimamizi wa mashine hizo.
“Tumefanya uhamasishaji kwa maofisa wa Tamisemi ili watambue maeneo ambayo mashine hizi zinapaswa kuwepo kisheria na waweze kubaini zile zinazofanya kazi kinyume cha sheria,” amesema.