Geita kuvuna pamba mbegu kilo 6.7 milioni

Wakulima wa zao la pamba Wilaya ya Geita wakiwa kwenye kikao cha tathmini ya zao hilo kwa msimu wa mwaka 2021/23 na maandalizi ya ununuzi wa pamba mbegu msimu wa mwaka 2023/24 kilichofanyika mjini Geita.

Muktasari:

Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji zaidi ya Sh216 milioni za ushuru zinatarajiwa kukusanywa kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na Sh138.5 milioni zilizokusanywa msimu uliopita.

Geita. Wilaya ya Geita inatarajia kuvuna zaidi ya kilo 6.7 milioni za pamba mbegu katika msimu wa 2023/24 ikiwa ni ongezeko la zaidi ya kilo 3.4 milioni zilizovunwa msimu uliopita wa 2021/22

Ofisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Richard Kapyela ameyasema hayo wakati wa kikao cha tathmini ya kilimo cha pamba kwa msimu wa 2021-2023 na maandalizi ya ununuzi wa pamba mbegu kwa msimu wa 2023/24 kilichofanyika mjini Geita.

Amesema kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji zaidi ya Sh216 milioni za ushuru zinatarajiwa kukusanywa kiasi ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na Sh138.5 milioni zilizokusanywa katika msimu uliopita.

Amesema pamoja na mafanikio hayo bado wakulima wanakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo mashambulizi ya wadudu waharibifu kama vile chawajani na vithrip pamoja na shambulizi ya ugonjwa wa mnyauko fuzari uliosababisha wakulima kung’oa mimea iliyoathirika.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amesema katika msimu ujao Wilaya hiyo haitatoa kibali cha ununuzi wa pamba kwa kampuni yoyote ya ununuzi itakayokuwa haijaandaa shamba darasa kwa ajili ya kutoa elimu ya kilimo bora cha zao hilo kwa wakulima

“Kila kampuni inayoshiriki kwenye ununuzi lazima iwe na shamba darasa kuwasaiida wakulima kupata elimu ya kilimo bora cha zao hilo mimi niwepo au nisiwepo lakini maandishi haya yatakuwepo ofisini na wataalamu msimamie hili hakuna atakaepata kibali cha kununua pamba kama hajaonyesha shamba darasa lake,”amesema Magembe

Aidha amekemea tabia ya wanunuzi wa pamba kushusha bei ya zao hilo baada ya kununua kutoka kwa wakulima na kusema katika msimu huu Serikali haitakubaliana na utetezi wa kushuka kwa bei katika soko la dunia na kuwataka kuheshimu makubaliano wanayoingia na wakulima wakati wa ununuzi.

Mmoja wa wakulima wa zao la Pamba katika kijiji Bukondo wilayani Geita, Samuel Kahindi amesema bei ya ununuzi ya Sh1700 kwa kilo moja ya pamba mbegu ni ndogo isiyoendana na gharama wanazotumia kwenye kilimo jambo linalowakatisha tamaa wakulima kuendelea kulima zao hilo.