GGML na tuzo inayobeba dhamira ya kuendeleza uhifadhi wa mazingira na usalama kazini

Wafanyakazi wa GGML wakiwa katika picha ya pamoja. Idadi kubwa ya Wafanyakazi wa kampuni ya GGML ni Watanzania_

Muktasari:

  • Halikuwa jambo la kushangaza sana Februari 22, mwaka huu wakati wa Kongamano la tatu la Kimataifa la Uwekezaji na Uchimbaji wa Madini ambapo maelfu ya washiriki waliposhuhudia Makamu Rais wa Kampuni Geita Gold Mining Limited (GGML) anayeshughulikia Maendeleo Endelevu, Simon Shayo akipokea tuzo tano ikiwemo ile ya mshindi katika kipengele cha mgodi uliozingatia Zaidi uhifadhi wa mazingira na usalama kazini kwa mwaka 2019/2020.

Halikuwa jambo la kushangaza sana Februari 22, mwaka huu wakati wa Kongamano la tatu la Kimataifa la Uwekezaji na Uchimbaji wa Madini ambapo maelfu ya washiriki waliposhuhudia Makamu Rais wa Kampuni Geita Gold Mining Limited (GGML) anayeshughulikia Maendeleo Endelevu, Simon Shayo akipokea tuzo tano ikiwemo ile ya mshindi katika kipengele cha mgodi uliozingatia Zaidi uhifadhi wa mazingira na usalama kazini kwa mwaka 2019/2020.

Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa wakati huo akiwa Makamu wa Rais alikabidhi tuzo hiyo mbele ya wadau waliokuwa wamejitokeza kushiriki Kongamano kuu la Tatu la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini mwaka 2021.

Tunasema jambo hili halikuwa jambo la kushangaza kutokana na ushiriki wa kampuni ya GGML katika miradi mbalimbali ya uhifadhi wa mazingira ndani na nje ya migodi yake huku ikizingatia suala la usalama wa wafanyakazi wake kwa kiwango cha juu.

Afisa uokoaji kutoka GGML Eric Lumbagi akitoa mafunzo ya jinsi ya kuzima moto ukiwa nyumbani. GGML hutoa elimu mbalim-bali za usalama katika jamii ya Mkoa wa Geita

Kwa mujibu wa GGML,Mgodi wa Geita una jumla ya wafanyakazi 5,349, ikiwa ni pamoja na wale waliojiriwa moja kwa moja na Kampuni na wale walio chini ya wakandarasi na watoa huduma mbalimbali.

Asilimia 98 ya wafanyakazi wote ni Watanzania. Katika Tuzo ya Mwajiri Bora wa mwaka chini ya Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), GGM ilishika nafasi ya kwanza mwaka 2018, ikiwa ni pamoja na kuwa mshindi katika kipengele cha usalama na afya kazini.

Katika tukio hilo, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) aliyekuwa anasimamia wizara yenye dhamana ya uhifadhi wa mazingira alisisitiza uhifadhi wa mazingira hoja inayoendelea kutekelezwa na GGM kwa miongo miwili sasa tangu ilipoanza uzalishaji wake.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Shayo alisema GGM inatiwa moyo na kitendo cha Serikali kutambua mchango wake katika nyanja za mazingira na usalama, uwekezaji kwenye jamii, ulipaji kodi kwa wakati na kiwango sasa, uwezeshaji wa wazawa na hivyo kuwa mshindi wa jumla wa sekta kwa mwaka 2019/2020.

Wafanyakazi wa GGML wakiwa katika picha ya pamoja. Idadi kubwa ya Wafanyakazi wa kampuni ya GGML ni Watanzania_

Alisema, “Tutaendelea kufanya kazi ya uchimbaji kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira na manufaa kwa jamii na nchi”.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodini na Nishati Tanzania (Numet), Nicomedes Kajungu anasema GGM ikiwa kinara lakini pia migodi mingine mikubwa imekuwa ikijitahidi zaidi katika suala la usalama mahali pa kazi.

Anasema wana mifumo sahihi ya kulinda afya za wafanyakazi.Kajungu anashauri uongozi wa GGM usibweteke na mafanikio ya kutambuliwa kwa tuzo hiyo na badala yake iwe chachu inayojenga hamasa ya kuendelea kufanya vizuri zaidi. Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 imeweka bayana majukumu ya mwajiri kuhusiana na usalama na afya mahali pa kazi.

Hata hivyo, majukumu yafuatayo ni muhimu kuzingatiwa:

• Kuhakikisha mahali pa kazi ni salama na kuwalinda wafanyakazi dhidi ya ajali, majeraha na madhara ya kiafya yanayoweza kuzuilika. Hii ni pamoja na kufanya mabadiliko katika muundo, michakato na mazingira ya kazi, kama vile, kupunguza kiwango cha kemikali na vihatarishi vingine vinavyoweza kuwaathiri wafanyakazi, kufuatilia madhara yatokanayo na vitu hivyo na kuweka kumbukumbu.

• Kuanzisha, kupitia na kuwasilisha taratibu za kazi kwa wafanyakazi ili wafuate mahitaji ya usalama na afya.

• Kuwapatia wafanyakazi wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi ulinzi wa kutosha na vifaa kinga vinavyohitajika. Hii ni pamoja na kutoa vifaa kinga kama vile vifunika uso, glovu na vifaa dhidi ya kelele, kutumia kemikali ambazo hazina madhara makubwa kiafya au kuboresha mzunguko wa hewa safi.

• Kuhakikisha usalama wa mazingira ya kazi kwa wafanyakazi na watu wengine wanaotembelea mahala pa kazi.

• Kubandika mabango, lebo na maelekezo yenye alama au taratibu zilizo rahisi kueleweka kuhusu namna ya kuzuia na kushughulikia ajali na majeraha au dharura mahali pa kazi baada ya tukio.

• Kuhakikisha wafanyakazi wanatumia vifaa vilivyo salama na kuvifanyia matengenezo vifaa hivyo.

• Kutoa mafunzo ya usalama kwa wafanyakazi kuhusu mbinu mahususi za kuhakikisha usalama na afya katika lugha ambayo wanaielewa.

• Kufanya vipimo na uchunguzi wa afya wa wafanyakazi kama ilivyoelekezwa na sheria hii kwa ajili ya kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa katika hali inayowawezesha kufanya kazi na kutunza afya na ustawi wao.

• Kuweka kumbukumbu sahihi zinazohusu majeraha na magonjwa yanayotokana na kazi.

• Kutoa taarifa OSHA kuhusu ajali au magonjwa yanayotokea katika maeneo ya kazi.

• Kusaidia wafanyakazi watumie haki yao ya kutoa taarifa kuhusu majeraha, ugonjwa au kifo vinavyotokana na kazi.

GGML na Mazingira

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 inaeleza wazi wajibu na majukumu ya wadau mbalimbali kuanzia serikali za mitaa hadi Taifa.

Mambo yanayosisitizwa katika Sheria hiyo ni mipango na usimamizi wa matumizi endelevu ya mazingira, kudhibiti uchafuzi wa mazingira, utunzaji wa taarifa na takwimu za mazingira, utafiti na ushiriki wa jamii na utekelezaji wa majukumu yatokanayo na mikataba ya kimataifa.

Pia, suala la utii na utekelezaji wa sheria pamoja na matumizi ya dhana mbalimbali za kusimamia hifadhi ya mazingira hususani Tathimini ya Athari katika Mazingira (TAM), Tathmini ya Mazingira Kimkakati (TMK), dhana za kiuchumi na viwango vya mazingira. Aidha kanuni, miongozo na programu mbalimbali zimetungwa ili kufanikisha utekelezaji wa sheria hiyo.

Kwa kutambua unyeti wa mazingira nchini, GGML imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya mazingira au kuunga mkono juhudi za wadau wengine wanaoanzisha harakati za uhifadhi wa mazingira Tanzania.

Kwa upande uwekezaji kwenye jamii, GGML imekuwa ikitumia zaidi ya TZS 10 bilioni kila mwaka kwaajili ya kuendeleza miradi ya jamii haswa katika maeneo ya afya, mazingira, elimu, kilimo na miundombinu, yote ikiwa ni sehemu ya Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii.