GGML ni mwekezaji anayejivunia kuwa mlipaji kodi bora Tanzania

GGML ni mwekezaji anayejivunia kuwa mlipaji kodi bora Tanzania

Muktasari:

  • Kampuni ya AngloGold Ashanti (AGA) imeendelea kuwa chachu ya matokeo chanya nchini Tanzania. AGA imekuwa mfano wa kupigiwa upatu katika sekta ya uziduaji kupitia uwekezaji na ubunifu wa nguvu kazi yake kwa jamii unaojitafsri kuwa maendeleo endelevu kwa jamii na faida kwa Taifa.

Kampuni ya AngloGold Ashanti (AGA) imeendelea kuwa chachu ya matokeo chanya nchini Tanzania. AGA imekuwa mfano wa kupigiwa upatu katika sekta ya uziduaji kupitia uwekezaji na ubunifu wa nguvu kazi yake kwa jamii unaojitafsri kuwa maendeleo endelevu kwa jamii na faida kwa Taifa.

Kampuni hiyo ambayo imekuwa ikiendesha Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM) wenye miongo zaidi ya miwili tangu uanze rasmi uzalishaji mwaka 2000 umekuwa ukijiendesha kwa ufanisi wa hali ya juu na kuzalisha bidhaa hiyo ya dhahabu pamoja na kulipa kodi kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Hatua hiyo ni moja ya mbinu zinazosaidia Tanzania kuchochea utekelezaji wa malengo yake ya maendeleo. Dira ya Taifa ya mwaka 2025 imeweka lengo la kuhakikisha sekta ya madini inachangia walau asilimia 10 ya pato ghafi la Taifa ifikapo 2025.

Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, madini ya dhahabu yanachukua asilimia 86 ya madini yote yanayozalishwa nchini na mgodi wa GGM ndiyo unaongoza kwa uzalishaji wa madini hayo kwa wingi takribani kila mwaka.

Kufikia mwaka 2020 mgodi wa GGM umeshafanya malipo ya Dola za Kimarekani 1.7 bilioni kwa Serikali kupitia kodi, mrabaha na riba mbalimbali.

Mchanganuo unahusisha mirabaha iliyolipwa ni Dola za Kimarekani 454 milioni, kodi zinazotokana na malipo ya wafanyakazi Dola 205 milioni, kodi ya mapato Dola 668 milioni, malipo ya leseni ya uchimbaji Dola 12 milioni, kodi ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi Dola 125 milioni na tozo ya huduma kwa Halmashauri za Geita Dola 14 milioni.

Soko la wafanyabiashara wadogo la Katundu lililojengwa na GGML kupitia fedha za uwajibikaji wa kampuni kwa jamii (CSR)_

Kwa mujibu wa Geita Gold Mining Limited (GGML), mwaka 2019 GGML ililipa kodi kiasi cha Sh467 bilioni sanjari na kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 5,000.

Ulipaji kodi wa GGML unaakisi malengo na mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa uliopanda kutoka asilimia tatu hadi asilimia 4.8 mwaka 2018 wakati malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ni kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Anglo Gold Ashanti, Christine Ramon anasema, “Katika ulimwengu wa sasa sio rahisi kuendesha kampuni ya uchimbaji, lakini tunahakikisha uwekezaji endelevu wa mabilioni, utekelezaji wa shughuli za maendeleo pamoja na ulipaji wa kodi halisi kwa Serikali ya Tanzania,” anasema kuwa, GGML inajivunia kuwa mlipa kodi bora na mkubwa nchini.

Baada ya kumalizika kwa kongamano la tatu la kimataifa la uwekezaji katika sekta ya madini nchini mwaka 2021, Makamu wa Rais wa GGML anayeshughulikia miradi endelevu, Simon Shayo alitoa ufafanuzi kwa nini mgodi huo umeshinda tuzo ya kuwa mlipaji kodi kinara wa sekta ya madini katika mwaka wa 2019/20 ikiwa ni pamoja na tuzo ya usalama na mazingira, tuzo ya mlipa kodi bora, tuzo ya mchangiaji bora wa huduma za jamii, mshindi wa pili wa tuzo ya ushirikishwaji wazawa na hivyo kuwa mshindi wa jumla.

“GGML imeshinda tuzo hizo kwa sababu ni kampuni inayozingatia uchimbaji endelevu ikiwa ni pamoja na unufaishaji wa jamii. Tunu yetu kubwa; jamii inayozunguka mgodi wowote wa AngloGold Ashanti inapaswa kunufaika kutokana na uchimbaji madini, imekuwa dira kuu ya kampuni ya GGML kuhakikisha tunashirikiana na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali inayonufaisha jamii hususan katika miundombinu na huduma za afya, elimu, maji, barabara na miradi ya kipato. Uwazi na uwajibikaji wa kampuni yetu katika utekelezaji wa sheria na miongozo kutoka serikalini ndio unaotufanya tuwe mstari wa mbele kulipa kodi na tozo za Serikali na kuongeza mapato ya Serikali,” anasema Shayo.

Lango la Shule ya Sekondari Wasichana ya Nyankumbu iliyojengwa na GGML kusaidia watoto wa kike ambao walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda shule_

Swali:Tuzo hizo zinatoa mwelekeo gani kwa GGML kwa uzalishaji wake katika misimu ijayo?

Shayo: Tuzo hizo zinatoa chachu ya kuendelea kufanya uzalishaji na tija katika misimu ijayo kwa sababu zinatoa hamasa na motisha mzuri zaidi wa kuendeleza rekodi hiyo.

Swali:Je, GGML kwa kiwango gani inazingatia malengo ya kitaifa kupitia shughuli zake za uzalishaji?

Shayo: GGML inazingatia malengo ya kitaifa katika shughuli zake kwa kuwa ndiyo dira na mwongozo wa Serikali. Tunavyochangia mapato mengi ya Serikali maana yake tunatoa mchango pia hata katika malengo ya Taifa kuufikia uchumi wa kati na kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 mchango wa sekta ya madini unafikia asilimia 10.

GGML ni mwekezaji anayejivunia kuwa mlipaji kodi bora Tanzania

Swali:Ni kwa namna gani GGML inajenga uaminifu kwa Serikali na Watanzania kupitia mchango wake kwa ujumla?

Shayo: GGML inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kila tunachofanya kinajikita katika uzingatiaji wa sheria, uwazi na uwajibikaji ndio hasa unaolenga uaminifu kwa Serikali. Ukifika kwenye ofisi zetu utagundua kuwa tunazo ofisi za Serikali zikiwemo ofisi za maofisa wa TRA na maofisa madini wakazi ambao wana ofisi zao mgodini kwa nia ya kutukagua na kufuatilia uwazi wa shughuli zetu. Hata tunaposafirisha dhahabu, maofisa wa Serikali huwepo na kutoa ripoti ya tozo na kodi mbalimbali za Serikali. Kila kitu kinafanyika kwa uwazi.