Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gofu kuunga mkono juhudi za Serikali kutunza mazingira

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imeweka mkakati wa kupanda hekta milioni 5.2 za miti na kulinda misitu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika (AU) ya utunzaji misitu na ardhi.

Dar es Salaam. Mashindano ya gofu ya NCBA msimu huu yamedhamiria kuunga mkono kampeni ya Serikali ya utunzaji wa mazingira kwa lengo la kupanda miti 6,000 nchini Tanzania ambapo wameanza na miti 1,000 Arusha.

Hayo yamebainishwa katika uzinduzi wa msimu wa pili wa mashindano ya gofu yanayodhaminiwa na Benki ya NCBA Tanzania ambapo mwaka huu yamelenga kuinua mchezo huo.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa, na Michezo, Dk Damas Ndumbaro, ambaye alihudhuria tukio hilo kama mgeni rasmi, na pia alishiriki katika mchezo wa gofu, amesema, “Serikali imefurahishwa kuona Benki ya NCBA ikichukua jukumu la msingi katika kuinua mchezo wa gofu Tanzania.

“Mpango huu, ukijumlisha na upandaji wa miti, sio tu unakuza mchezo huu peke yake, lakini unachangia katika juhudi za utunzaji wa mazingira, ikionyesha kuwa michezo inaweza kuleta mabadiliko chanya."

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Claver Serumaga, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika dhamira moja.

“Kupitia ushirikiano wa mpango wetu wa gofu pamoja na juhudi za upandaji miti, tunaonyesha kujitolea kwetu kwenye mipango ya Serikali katika utunzaji wa mazingira”.

Ukiachana na kutunza mazingira, mashindano ya gofu, NCBA imejipanga kuwaleta pamoja wachezaji, mashabiki na wadau wa gofu na kuzidisha ushirikiano kati ya benki hiyo na wateja wake.

Hivi karibuni Serikali ya Tanzania iliweka mkakati wa kupanda hekta milioni 5.2 za miti na kulinda misitu ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika (AU) ya utunzaji misitu na ardhi.

Mpango huu ni sehemu ya juhudi za kuokoa hekta milioni 100 za misitu barani Afrika kufikia mwaka 2030, ulioahidiwa na nchi 34 za Afrika mwaka 2015.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, alisema Tanzania imefanikiwa kupanda hekta milioni 2.4, sawa na asilimia 46 ya lengo lake.

Akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa nane wa AFR100 ulioandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya AUDA-NEPAD na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Waziri Kairuki alibainisha umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa miti katika kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.