GSM atoa vielelezo umiliki wa ardhi, Makonda amjibu

Muktasari:

  • Wakati Wakili wa mfanyabiashara maarufu nchini, Ghalib Said Mohamed (GSM), Alex Mgongolwa ameweka wazi vielelezo vya umiliki wa eneo kiwanja namba 60 lililopo Regent Estate Kinondoni jijini hapa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda amemtaka mfanyabiashara hiyo kumwachia mali yake.


Dar es Salaam. Wakati Wakili wa mfanyabiashara maarufu nchini, Ghalib Said Mohamed (GSM), Alex Mgongolwa ameweka wazi vielelezo vya umiliki wa eneo kiwanja namba 60 lililopo Regent Estate Kinondoni jijini hapa, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amemtaka mfanyabiashara huyo kumwachia mali yake.

Mzozo wa kiwanja hicho umeibuka hivi karibuni, ambapo Makonda ameonekana katika video iliyorushwa kwenye mitandao ya kijamii akisisitiza kuwa eneo hilo ni lake.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Machi 12, 2022 jijini hapa Wakili Mgongolwa amemtaka mtu ambaye hakumtaja kwa jina, kuweka wazi vielelezo vya umiliki  alivyonavyo vya  eneo hilo na vielelezo kutoka Wizara ya Ardhi vinavyompa uhalali .

Hata hivyo, Makonda alipotafutwa kwa simu leo, amejibu kwa ujumbe wa WhatsApp, akisema; “GSM usinilazimishe kusema uozo wako achia mali yangu. Walioko nyuma yako nawajua.”

Kama hiyo haitoshi, katika ukurasa wake wa Instagram, Makonda aliweka video ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka ambayo pamoja na mengine alieleza haja ya kutaka Jeshi la Polisi kuchunguzwa, kisha akaweka ujumbe:

“Naunga mkono hoja ya Kamati Kuu, ya kuchunguza mwenendo wa baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi, wanaolipaka tope Jeshi la Jolisi kwa kuwalinda wafanyabiashara MATAPELI wanaodhulumu mali za watu. Naomba tuanze na Dar es salaam na mimi Paul Makonda niko tayari kutoa ushirikianao.”

Madai ya GSM

Akifafanua zaidi kuhusu umiliki wa ardhi hiyo, Wakili Mgongolwa amesema, mteja wake Ghalib Said Mohamed alinunua ardhi wilaya ya Kinondoni, eneo la Regent Estate plot no. 60, title no. 186153/60, kwa lengo la ujenzi wa makazi Novemba 21, 2006."

Vilevile, Mgongolwa amesema Septemba 2017, mteja wake aliingia mkataba na kampuni ya ujenzi iitwayo Group Six International (Contract Class One) kwa ajili ya ujenzi wa eneo hilo wenye thamani ya Sh640 milioni.

"Ghalib aliomba kibali cha ujenzi na Manispaa ya Kinondoni walitoa kibali hicho Oktoba 16, 2017 chenye kumbukumbu namba 00020032 kwa Ghalib Said Mohammed kwa ajili ya ujenzi eneo hilo," amesema.

Ameongeza kuwa baada ya kibali hicho kutoka, Group Six walianza ujenzi na walipeleka malipo ya awali ya ujenzi Januari 31, 2018 huku mteja wake huyo akitekeleza sehemu ya mkataba kwa kulipa kiasi cha Sh51.92 milioni, malipo ambayo amedai yana uthibitisho kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

"Mimi leo nathibitisha uhalali wa miliki, unaweza ukawa na uhusiano na mtu lakini sio wa kibiashara wa kuuziana na kuhamishiana miliki licha ya kuingia katika makubaliano ya kuhamishiana miliki,"

Mgongolwa amesema kufahamiana na mtu ni jambo lingine na miliki ni jambo lingine, hivyo ushahidi wa vielelezo kisheria unakingwa na vielelezo hivyo.

"Tunatoa changamoto kwa mtu yoyote yule aje akinzane na vielelezo vyetu, huu ni ujenzi kwa mujibu wa mkataba na haujasimamiwa na mjomba au shangazi.

"Yoyote yule anayesema ardhi ni ya kwake iwe kimahusiano au lah, aje na vielelezo kwetu, mtu mwenye dhana tofauti milango ya mahakama iko wazi, ila kwa sasa hawatakwenda mahakamani.

"Hatua tutakazozichukua kuanzia sasa itategemea na matukio ambayo yatafuata kwani ndiyo yatatupa mwongozo wa nini tukifanye, ikitokea hatua ya kwenda mahakamani tutakwenda, ikitokea kuangalia ngazi nyingine tutalipeleka kwa kuwa maelekezo yetu yako wazi tunatakiwa kulinda haki ya mteja wetu sambamba na jina lake," amesema.