Gyumi: Serikali isitishe ununuzi wa mashangingi, inunue pedi shuleni

Muktasari:

  • Wakati kukiwa na wasichana wengi wanaoacha shule kutokana na sababu mbalimbali, mwanaharakati na mwanasheria Rebecca Gyumi ameishauri Serikali kuangalia namna ya kupunguza Sh68 bilioni kutoka kwenye Sh558 bilioni zinazotumika katika ununuzi wa magari kwa mwaka ili zinunue taulo na kuzigawa bure kwa wasichana wote shuleni.

Dar es Salaam. Mwanaharakati Rebecca Gyumi amesema Serikali iangalie namna ya kuanzisha jitihada za kuwafanya watoto wa kike wabaki shuleni kwa kutoa taulo za kike bure.

Amesema kiwango cha kodi ambacho Serikali inapata kwa kutoza kodi kwenye taulo hizo ni Sh3 bilioni, ambayo ni sawa na magari matano yanayonunuliwa kwa ajili ya watumishi wa Serikali kila mwaka.

Gyumi ameyasema hayo leo Jumatano, Machi 20, 2024 alipokuwa anachangia mjadala wa Mwananchi Space uliokuwa unarushwa mubashara kupitia mtandao wa X ukiwa na mada iliyokuwa inahoji, ‘Nini matarajio yako kwa kipindi kilichobaki cha uongozi wa Rais Samia?’

Amesema Serikali kama itaamua kwa mwaka kugawa taulo za kike bure kwa wanafunzi shuleni itatumia Sh68 bilioni tofauti na magari yanayonunuliwa kila mwaka kwa Sh558 bilioni.

“Ukifanya hesabu hiyo Sh68 bilioni ikipelekwa kusaidia wanafunzi kubaki shule ni sawa na asilimia 12 ya bajeti inayotumiwa na Serikali kununua magari, kimsingi unaweza kusema ni sawa na magari 13 tu ambayo Serikali inaweza kusema hainunui ili watoto wetu waende shule wakiwa na furaha,” amesema Gyumi.

Akichangia mada hiyo, Mjumbe wa Kamati Kuu na Msemaji wa Sekta ya Afya ACT, Dk Elizabeth Sanga amesema upatikanaji wa huduma za afya na ugharamiaji wa huduma ni matarajio ya walio wengi.

“Katika eneo la ugharamiaji huduma za afya bado kuna tatizo, kwa sababu mfumo uliopo si rafiki kwa Mtanzania aliyepo kwenye sekta isiyokuwa rasmi.

“Wanashindwa kumudu gharama za bima ya afya na asilimia 80 hawapo kwenye mfumo wa bima hivyo, wakiugua wanajilipia kutoka mifukoni mwao,” amesema.
Dk Sanga amesema ili kubadilisha hilo, ACT Wazalendo wamekuwa wakipendekeza lakini bado kuna kusuasua hasa katika mfumo wa NHIF ambao haujawa na ufanisi, katika ugharamiaji wa huduma za afya.

Akichokoza mada hiyo, Mhariri wa Jarida la Afya gazeti la Mwananchi, Herieth Makwetta alisema Watanzania bado wana matarajio makubwa ya utekelezwaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo Rais ameisaini Desemba, 2023.

“Ni historia kubwa lakini matarajio ni namna itakavyotekelezwa ili wale waliokuwa wanategemea fedha za mfukoni kujitibu wasiingie katika umasikini pindi wanapougua,” amesema.

Amesema japokuwa kuna mafanikio mengi hasa miaka mitatu kwa kuongeza idadi ya vituo vya afya, huduma za dharura kwa kujenga majengo mapya katika halmashauri 82 na majengo ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa ajali 105 kutoka 7 mwaka 2020, matarajio ya Watanzania wengi ni kuzidi kuongeza ikama ya watumishi kwa maana ya rasilimali watu.

“Majengo na vifaa pekee ni mwanzo mzuri, lakini bado wengi wanatamani wakienda kituo cha afya wakutane na watoa huduma, wapate huduma waliyoitarajia. Miaka mitatu Rais Samia ameajiri watumishi 35,450 ni mwanzo mzuri,” amesema.
Ametaja eneo jingine lenye changamoto kubwa ni Sera ya Afya ya mwaka 2007,

“Matarajio ya wengi sera hii itekelezwe, bado kuna changamoto katika matibabu ya wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee. Uchangiaji wa huduma unatajwa eneo hili, Watanzania wengi wanatarajia lifanyiwe marekebisho au Sera hii ihuishwe upya.”