Hakimu Tabora awataka wazazi kuwakagua watoto sehemu za siri

Muktasari:

  • Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto, wazazi wameshauri kuwa na tabia ya kuwakagua watoto wao wanapotoka shule. Hakimu mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Jovit Katto amesema hali ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto kwa sasa ni mbaya na hatua za kudhibiti hali hiyo lazima zichukuliwe.

Tabora. Kutokana na kukithiri kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto, wazazi wameshauri kuwa na tabia ya kuwakagua watoto wao wanapotoka shule.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Jovit Katto amesema hali ya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto kwa sasa ni mbaya na hatua za kudhibiti hali hiyo lazima zichukuliwe.
Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa umma katika wiki ya sheria, hakimu Katto amesema wazazi wanapaswa kuwakagua watoto wao wanapotoka shule na hasa kwa wale wanaotumia usafiri wa bodaboda na bajaji waendapo au kurudi shuleni.
Ameeleza kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kulawitiwa jambo ambalo linaendelea kukua siku hadi siku huku watoto wakiathiriwa na matukio hayo.
"Kumekuwa na ongezeko kubwa la kesi za ulawiti dhidi ya watoto jambo ambalo linapaswa kushughulikiwa ili kulimaliza," amesema.
Mkazi wa Mtaa wa Rehani Kata ya Ng'ambo, Mwajuma Athuman ameunga mkono wazazi kuwakagua na kuwaogesha watoto wao, akisema ni jambo zuri kwa mzazi kufahamu baadhi ya mambo.
"Yupo mwenzetu mmoja baada ya kumuona mwanaye hayupo katika hali nzuri, alimkagua wakati wa kumuogesha na kubaini kafanyiwa kitendo cha ukatili," amesema.
Mwendesha bodaboda Rajab Maulid amesema wapo wenzao wachache wanaowaharibia kwa kwenda kinyume na kuwafanyia ukatili watoto.
"Baadhi yetu tunapewa jukumu la kuwapeleka watoto shule na kuwarudisha, sasa wakitokea wachache wanaokwenda kinyume kwa kweli wanatuharibia," amesema.
Wazazi na walezi hasa katika Manispaa ya Tabora, baadhi wanawatumia bodaboda na bajaj, kuwapeleka watoto wao shuleni na kuwafuata, wakilipana kwa wiki au mwezi kutegemeana na makubaliano.