Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hali ilivyo maeneo mbalimbali Dar

Muktasari:

  • Mwananchi limepita maeneo mbalimbali na kushuhudia utulivu. Hakuna cha foleni na hata usafiri kama daladala ni chache barabarani. Hii inatokana na tishio la uwepo wa maandamano huku Serikali ikionya yeyote atakayejaribu kuandamana hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Dar es Salaam. Kutokana na mvua ya manyunyu iliyoanza kunyesha alfajiri ya leo Jumanne, Julai 7, 2026 jijini Dar es Salaam, baadhi ya maeneo yamekuwa tulivu, maduka yakichelewa kufunguliwa, usafiri barabarani ukiwa mchache huku ulinzi ukiimarishwa.

Dar es Salaam yenye hekaheka nyingi, hali hiyo ni tofauti. Hadi saa 4 asubuhi hali imekuwa tulivu, vikosi vya ulinzi na usalama vimetanda maeneo mbalimbali mathalani kwenye makutano ya barabara, miundombinu kama mwendokasi, madaraja na ofisi nyeti.

Mwananchi limepita maeneo mbalimbali na kushuhudia utulivu. Hakuna cha foleni na hata usafiri kama daladala ni chache barabarani. Hii inatokana na tishio la uwepo wa maandamano huku Serikali ikionya yeyote atakayejaribu kuandamana hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Mabibo Sokoni na Shekilango ambapo kunauzwa bidhaa za vyakula, watu ni wachache tofauti na ilivyozoeleka. Pia, baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta mpaka saa 4 kasoro vingi vilikuwa vimefungwa na mtu aliyekuwa akisogea kuhitaji huduma alielezwa bado hawajafungua.

Akizungumza na Mwananchi, katika Kituo cha Tangi Bovu, Maliki Simba amesema kula yake hutegemea kupiga debe na kubeba mizigo ya abiria sasa leo mpaka saa 2:30 asubuhi hakuna abiria wa mizigo waliotoka sokoni.

“Tumekaa kijiweni tunapiga debe lakini abiria sio wengi kama kawaida na kama hali itaendelea hivi nikipata pesa ya chai itabidi niondoke nyumbani,” amesema Simba.

Naye Dereva wa bajaji katika eneo la Mwenge Stendi, akizungumza kwa sharti la kutotaja jina lake amesema hapo kituoni leo Jumanne bajaji ambazo hazina usajili wa kituo hiki tumeziona nyingi zikisubiri abiria na kuashiria hao madereva siyo wa hapo.

Amesema wengi wao wameingiwa hofu na kuamua kuondoka kurudi nyumbani.

Amesema hata yeye huamka saa 10 alfajiri lakini leo ameingia kijiweni kwa kuchelewa muda wa saa 3 asubuhi.

“Kuna abiria nampeleka hospitali kuchukua dawa, baada ya hapo narudi nyumbani sitaki shida na mtu,” amesema.

Katika maeneo ya Temeke, baadhi ya wananchi wameonekana kwa uchache wakiendelea na shughuli zao katika maeneo kadha ya Temeke huku hali ya utulivu, kimya na amani ukionekana mitaa ya Temeke, Tandika, Yombo na Buza.

Hali hii ni tofauti na ilivyokawaida kwani hata katika maeneo muhimu kama Tandika sokoni, biashara zimeonekana kuanza kwa kusuasua tofauti na kawaida ambapo barabara za Tandika hufurika wafanyabiashara, bajaji na daladala.

Badala yake, maduka mengi yameonekana kufungwa, wafanyabiashara wachache wakianza kutandaza biadhaa zao katika maeneo kadhaa. Kwa upande wa barabara, zimesalia kuwa nyeupe tofauti na mazoea, bajaji na daladala chache zikionekana na abiria.

Aidha, maeneo ya Kimara kuanzia Kituo cha Mwendokasi Coner mpaka Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam, hadi saa 2:30 asubuhi, Mwananchi imeshuhudia magari na watembea kwa miguu wakionekana kwa uchache kuliko ilivyo kawaida.

Pia katika maeneo hayo shughuli nyingi za kawaida zikiendelea kwa tahadhari, hakuna msongamano mkubwa wa magari wala watu katika barabara na maeneo ya biashara kama siku zingine

Jana Jumatatu, Julai 6, 2026, Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam alisema nchi itaendelea kuwa salama, akisisitiza Serikali haipangiwi tarehe, iko tayari na imara wakati wote na katika maeneo yote.

Pia, alisema Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo yote, kuhakikisha kila anayestahili kwenda katika shughuli za kiuchumi anakwenda, anayepaswa kwenda shule, zitafunguliwa na atakwenda.

Alisema Serikali itachukua hatua zote stahiki kwa yeyote atakayetishia au kutenda kitendo chochote cha uhalifu au kutishia amani.