Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hali tete kwa wananchi kupambana na janga la corona

Muktasari:

  • Utekelezaji wa mwongozo wa pili wa udhibiti wa maambukizi ya Covid-19 katika taasisi za elimu nchini umeanza kwa kusuasua baada ya shule nyingi kutotekeleza maagizo huku hali ikiwa tete zaidi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) katika upimaji wa wasafiri wanaoingia.

Dar/Mikoani. Utekelezaji wa mwongozo wa pili wa udhibiti wa maambukizi ya Covid-19 katika taasisi za elimu nchini umeanza kwa kusuasua baada ya shule nyingi kutotekeleza maagizo huku hali ikiwa tete zaidi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) katika upimaji wa wasafiri wanaoingia.

Pamoja na jitihada za Serikali kutangaza kuwapo kwa ugonjwa huo, bado utaratibu wa udhibiti wa wageni wanaoingia kupitia JNIA umeonekana kuyumba kutokana na wingi wa wasafiri wanaokuja na ndege kutoka nje na wakitakiwa kupima.

Juzi Serikali ilitoa mwongozo unaowataka wanafunzi kujikinga na corona kwa kuvaa barakoa, kutumia maji tiririka na kunawa kwa sabuni pamoja na vitakasa mikono lakini ni vyuo vikuu zaidi ndivyo vinauzingatia.

Katika shule za msingi na sekondari hali ni tofauti kwani wanafunzi bado wamejazana darasani na hakuna anayevaa barakoa hasa katika shule za umma.

Baadhi ya shule za msingi jijini Dar es Salaam ikiwamo Diamond, Buza na Mbande zimeweka miundombinu rafiki kwa wanafunzi kunawa mikono na vitakasa mikono lakini nyingi bado hazijafanya hivyo.

Wanafunzi walioongea na gazeti hili walikiri hawafahamu kuhusu uvaaji barakoa huku wengine wakieleza maagizo waliyopewa na walimu wao.

“Tulivyofika asubuhi tumeelezwa namna ya kujikinga na corona na ugonjwa huu tumeambiwa upo. Walimu wamesema kesho tuje tumevaa barakoa,” alisema mmoja wa wanafunzi wa Shule za Msingi Mbande iliyopo wilayani Temeke.

Baadhi ya walimu waliohojiwa walisita kuzungumza na gazeti hili kwa madai kuwa hawajapewa ruhusa ya kufanya hivyo.

Baadhi ya shule mkoani Mwanza hazijazingatia maelekezo hayo na hakuna wanafunzi wanaovaa barakoa. Katika Shule ya Msingi Tambukareli iliyopo Butimba wanafunzi walionekana wakiwa wamesongamana huku hamna hata mmoja aliyevaa barakoa.

Hali hiyo ilionekana pia katika Sekondari ya Capripoint ambako wanafunzi hawakuwa na tahadhari yoyote dhidi ya virusi vya corona. Katika Sekondari ya Lake mabango ya tahadhari ya virusi hivyo yalionekana yamebandikwa katika kuta za madarasa yakihamasisha watumishi na wanafunzi kujikinga na janga hilo.

Akizungumza na Mwananchi, mkuu wa sekondari hiyo, Lucas Bunuma alisema miongoni mwa hatua walizochukua ni kuwataka wanafunzi kuvaa barakoa wakati wote na kuchukua tahadhari zote.

Wilayani Sengerema shule nyingi za msingi hazijachukua tahadhari yoyote ya kuwakinga wanafunzi dhidi ya virusi vya corona huku wazazi wakiiomba Serikali izidi kutoa elimu ya kutosha.

Mkoani Kilimanjaro Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU ) kimeendelea kuweka mkazo wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa kusema wanafunzi ambao hawatakavaa barakoa hawatoruhusiwa kuingia kwenye vipindi vyao darasani.

Daktari na katibu wa kamati ya ufuatiliaji ya mwenendo wa ugonjwa wa Covid-19 wa chuo hicho, Dk Mugisha Ntiyonza Nkoronko alisema wameweka mkazo kuhakikisha kila mwanafunzi na watumishi wote wanachukua tahadhari.

Abiria hawajali kujikinga

Hali ya kujikinga bado imeonekana kuendelea kupuuzwa katika maeneo yenye mikusanyiko hata katika stendi ya mabasi yaendayo mikoani.

Meneja wa Stendi ya Magufuli jijini Dar es Salaam, Maira Mkama alisema wametoa maelekezo kwa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) kuchukua tahadhari zote zinazopendekezwa.

Alisema Serikali ilishatoa maelekezo kwa wananchi kuhakikisha wanavaa barakoa wakati wote wanapokua kwenye mikusanyiko, kunawa mikono kwa maji tiririka na kutumia vitakasa mikono.

“Kwa upande wa stendi tumejitahidi kuweka maeneo maalum kwa ajili ya watu kunawa mikono, pia tumewaambia wenye mabasi kuendelea kuchukua tahadhari zote zilizoshauriwa na wataalamu wa afya,” alisema Mkama.

Mjumbe wa kamati tendaji ya Taboa, Mustafa Mwalongo alisema Serikali inapaswa kutoa elimu kwa kuwa watu wamejisahau na kupuuzia kuchukua tahadhari.

“Manispaa inapaswa kuweka matangazo na kutoa elimu kwa wananchi hasa uvaaji barakoa na unawaji mikono, katika awamu hii ya tatu mwamko ni mdogo sana,” alisema Mwalongo.

“Jukumu letu ni kuweka vitu vilivyo ndani ya uwezo wetu kwenye gari, mambo mengine ni jukumu la Serikali, katika maambukizi ya awamu ya kwanza elimu ilitolewa lakini awamu hii tunaona kuna tatizo kwenye utoaji wa elimu,” alisema.

Kasheshe la upimaji JNIA

Wakati Serikali ikiendelea kutoa miongozo ya kukabiliana na maambukizi ya Covid-19, kumekuwa na udhibiti mdogo JNIA ambalo ni miongoni mwa malango muhimu ya kuingilia watu nchini.

Kutokana na udhibiti mdogo uwanjani hapo, upo uwezekano wa kupitisha watu wenye ugonjwa huo au kuwa chanzo cha kuongeza kasi ya maambukizi mapya nchini.

Ingawa Wizara ya Afya iliagiza abiria wote wanaowasili nchini kupimwa Covid-19, jana hali ilikuwa mbaya uwanjani hapo hasa mchana wa Julai 3 baada ya kuwasili ndege tatu zilizofuatana na kusababisha msongamano mkubwa wa watu katika eneo lililotengwa kwa ajili ya kufanya vipimo.

Mmoja wa mashuhuda aliliambia Mwananchi juu ya kutofuatwa kwa hatua zinazoelekezwa kukabiliana na ugonjwa huo isipokuwa kuvaa barakoa ambalo ni sharti linalozingatiwa zaidi kuanzia kwenye ndege.

Wingi huo wa abiria ulionekana kuwazidi uwezo watoa huduma ya afya na kuwa chanzo cha utaratibu mbovu uliowasabisha mzozo huku watu wakilalamika kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu.

Wapo waliotumia mwanya huo kuvunja utaratibu na kuwafuata watoa huduma waliokuwa tayari kutoa vyeti bila kuwa na uhakika wa majibu ya kipimo kilichochukuliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Julius Ndyamukama alisema suala la corona linasimamiwa na Wizara ya Afya na ni changamoto hata kwao kwa kuwa linaleta usumbufu kwa abiria.

“Ni kweli jana (juzi) abiria walikuwa wengi waliongezeka sana, tulipata frustration kutokana na hali iliyokuwepo lakini suala la vipimo sio letu ni la Wizara ya Afya sisi tunafanya facilitation tu,” alisema.

Huku akisitiza kuwa chochote kuhusu hali hiyo waulizwe Wizara ya Afya, alidokeza kuwa changamoto anayoiona ni uchache wa wataalamu wa kutoa huduma na vifaa vya kufanyia kazi, vyote hivyo vinapaswa kuongezwa.

Alipotafutwa Mkuu wa Masuala ya Afya aliyepo JNIA, George Ndaki alisema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kuhusiana na suala hilo kwa kuwa kuna kikao kikubwa cha kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo.

“Kwa sasa siwezi kuongelea hilo kwa sababu kuna kikao kikubwa cha waganga wakuu na menejimenti kutafuta mwarobaini wa hilo baada ya hapo nitakupa msemaji wa wizara akupe taarifa,” alisema Ndaki.

Akizungumzia suala hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alikiri kuwapo kwa changamoto hiyo na Serikali imeanza kuifanyia kazi.

Profesa Makubi alieleza kuwa mganga mkuu wa Serikali alishinda uwanjani hapo kuweka mambo sawa. “Ni kweli kuna changamoto ambazo zimeendelea kujitokeza pale uwanjani lakini tunazishughulikia na tumefanya maboresho makubwa katika baadhi ya maeneo,” alieleza Profesa Makubi.

Hali ilivyokuwa

Chanzo chetu cha habari kiliwasili uwanjani hapo saa 2:25 mchana na moja kati ya ndege za mashirika matatu yaliyowasili mchana huo na kuelekea eneo lililotengwa kwa ajili ya vipimo ambako kilikuta umati mkubwa.

Kutoka kwenye ndege hadi eneo hilo hakukuwa na sharti la kunawa wala kutakasa mikono, huku sharti la kupeana nafasi likiwa halijazingatiwa kabisa kwani watu walisongamana kwenye foleni.

Katika dirisha la kwanza mgeni alihakiki fomu ya afya ambayo inapaswa kujazwa mtandaoni kisha kupimwa joto. Baada ya kujaza fomu hiyo na kupewa namba ya kulipia, foleni ya pili ni ya kulipia katika benki za NMB na CRDB. Baada ya kulipia kuna foleni ya tatu ya uhakiki wa malipo yaliyofanyika.

“Foleni ya nne ni kuelekea eneo la upimaji ambalo kwa siku hiyo lilikuwa na wataalamu watano waliokuwa wakifanya kazi hiyo huku ikielezwa kuwa majibu yanatoka dakika kumi. Niliingia saa 9:30 alasiri,” alieleza shuhuda huyo.

Shuhuda huyo alieleza utaratibu ulionekana kuwa mbovu zaidi kwenye utoaji majibu ambako hakukuwa na utaratibu uliopangwa hali iliyosababisha watu kurundikana sehemu moja na kumsonga ofisa aliyekuwa akiita majina ya waliopimwa.

Inaaminika mara kadhaa abiria walitaka kuanzisha vurugu kutokana na kutoridhishwa na utaratibu huo kwani wakati mwingine walijitokeza watu wawili wakiita majina katika maeneo tofauti hali iliyosababisha watu wasielewe wakae upande upi.

Shuhuda wetu alikaa eneo hilo hadi saa 10:07 jioni bila jina lake kuitwa na aliporudi eneo alilopimwa ofisa alimjibu “nenda kasubiri tunaendelea kujaza, vyeti vitaitwa. Nashindwa kukujazia sijui kama ni negative au positive.”

Wakati ofisa huyo akijibu hivyo, mwenzake aliyekuwa jirani akamwambia “mjazie hakuna (yaani hana tatizo) leo wote ni `negative’ (hawana tatizo).”

(Imeandaliwa na Herieth Makwetta, Fortune Francis, Janeth Joseph, Saada Amir, Daniel Makaka, Mgongo Kaitira, Habel Chidawali na Ephraim Bahemu).