Halima Mdee na wenzake waitwa kamati kuu Chadema

Wednesday November 25 2020
kina mdee pic
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya Chadema imewaita wanachama wao 19 ambao jana waliapishwa  na Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwa wabunge wa viti maalum ili wajieleze kuhusu aliyewateua.

 Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Novemba 25, 2020 na katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika aliyekuwa akizungumzia kitendo cha wanachama hao kula kiapo kuwa wabunge jana mjini Dodoma wakati orodha ya majina yao haikuteuliwa na Chadema wala kuwasilishwa na chama hicho Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Chama inabidi kichukue hatua kwa kuwa Chadema inaendeshwa kwa mujibu wa katiba, kanuni na maadili na itifaki. Katiba yetu imetoa mfumo kwamba jambo lolote linapotokea hatua zozote zisichukuliwe bila kuitwa wala kujieleza kwa kuwa ni la dharura.”

“Nawatangazia kuwa chama kitatumia utaratibu wa dharura katika kushughulika nalo kupitia kanuni ya 6.5 ya chama na kwa kuwa mamlaka ya jambo hili ni kamati kuu ya chama naomba niwaambie tumeitisha kikao cha kamati kuu ya chama kitakachofanyika Ijumaa Novemba 27,2020,” amesema Mnyika.

Amesema wanachama hao 19 wanatakiwa kufika makao makuu ya Chadema mtaa wa Ufipa jijini Dar es Salaam bila kukosa Ijumaa Novemba 27, 2020 saa 2:00 asubuhi kutoka popote pale walipo.

Amesema kifungu cha pili cha katiba ya Chadema, kamati kuu inaweza kuchukua hatua kama maslahi ya chama yanaweza kulaumiwa, hivyo pamoja na kuwa watawaandikia barua lakini wanatakiwa pia wapate taarifa kwa umma ili kuondoa visingizio kwamba hawakusikia.

Advertisement

Mnyika amesema kiapo cha wabunge hao sambamba na madai kuwa wameteuliwa hakina baraka za mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

“Ajitokeze mtu mmoja asema ni kikao gani kilichokaa cha kamati kuu ya chama au kiongozi mkuu kufanya uteuzi wa majina..., hakuna.  Kamati kuu haikukasimu wala hakuna chombo chochote kilichokaa.”

“Walioenda kuapa kimsingi  walijiteua..., kwenda kuhalalisha ubatili, uasi, usaliti na uharamu kwa kushiriki kiapo. Chama  kitachukua hatua gani si kazi ya katibu mkuu, kazi yangu ni kuhakikisha kamati kuu imeitishwa  kikao kikuu cha chama kitafanyika Ijumaa,” amesema Mnyika.


Advertisement